"Sina shaka naye!" Osoro aamini Arati atafanya kazi Kisii licha ya kurushiana ngumi awali

Miaka 2 iliyopita katika mazishi ya babake Joash Maangi, wawili hao walirushiana ngumi hadharani

Muhtasari

• Osoro ambaye aliyeuliwa kama mbunge kwa mara ya pili alisema hana shaka na Arati kwani atafanya kazi vilivyo Kisii.

Mbunge Slyvanus Osoro akimpongeza gavana Simba Arati wakati wa kuapishwa kwake.
Kisii Mbunge Slyvanus Osoro akimpongeza gavana Simba Arati wakati wa kuapishwa kwake.
Image: Facebook

Mbunge wa Mugirango Kusini Slyvanus Osoro amempongeza gavana mteule wa kaunti ya Kisii Simba Arati na kusema kwamba ana uhakika kaunti hiyo iko katika mikono salama na mbunge huyo wa zamani wa Dagoretti kaskazini ambaye sasa ni gavana wa pili wa Kisii.

Osoro amepakia picha kadhaa wakikumbatiana na Arati na kummiminia sifa tele licha ya wawili hao miezi kadhaa iliyopita kuzozana hadharani katika hafla ya mazishi na kurushiana ngumi huku wakitukanana vibaya.

Osoro ambaye alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa Arati Alhamis katika uwanja wa Gusii  alimtaja Arati kama mtu mwenye ukakamavu katika kazi yake na hata kutolea mifano kwamab wameshirikiana katika kamati mbali mbali za bunge na anajua uwezo wake katika kutekeleza majukumu ambayo wakaazi wa Kisii wamemtwika.

“Nimetumikia pamoja na gavana wetu mpya katika kamati kadhaa za Bunge na ninaweza kuwathibitishia kwa mamlaka, bila shaka kuwa, hakika yeye ni kiongozi MWENYE MAWAZO. Sina shaka na uwezo wake. BILA KUJALI itikadi za vyama vyetu, lazima tuungane mkono na kumuunga mkono gavana wetu mpya,” Osoro aliandika kupitia Facebook yake.

Osoro ambaye ni mtetezi mkali wa naibu rais anayeondoka William Ruto alikumbana katika vita vya ngumi na Arati ambaye anajulikana kuzitetea sera za kinara wa ODM Raila Odinga katika mazishi ya babake aliyekuwa naibu gavana wa kaunti hiyo Joash Maangi mwaka 2020.

Mbunge huyo aliwania kwa mara ya pili kama mbunge wa Mugirango Kusini kupitia tikiti ya chama cha UDA na kushinda huku Simba Arati akiwania ugavana kwa tikiti ya ODM na kushinda pia baada ya kuhudumu kama mbunge wa Dagoretti Kaskazini kwa miaka 10.