Wabunge wapya waliochaguliwa katika Bunge la Kitaifa wamepuuzili mbali uamuzi wa Mahakama ya Juu kuwa mfuko wa maendeleo ya jimbo (NGCDF) sio halali.
Wabunge hao waliapa kuwa, watahakikisha kuwa hazina hiyo imerejeshwa.Kwa pamoja walidai kuwa ni CDF ya 2013 ndiyo iliyokuwa kinyume cha sheria wala sio NGCDF.
Mnamo siku ya pili ya mkutano wa utangulizi bungeni, Wabunge hao walisisitiza kuwa watahakikisha hazina hiyo inarejeshwa.
Wabunge wanatafakari kuweka sheria mpya endapo NGCDF itachukuliwa kuwa kinyume na katiba.
Mwanasiasa mkongwe Julius Sunkuli ambaye ni Mbunge Mteule wa Kilgoris alishikilia kuwa hazina hiyo ambayo ilitajwa kuwa kinyume na Katiba inafaa kurejeshwa.
“Natumai sheria inaweza kutafsiriwa kwa manufaa ya hazina hiyo, bila CDF taifa hili litakuwa na matatizo. Watu wamezoea CDF na imechangia pakubwa kwa maendeleo na kuboresha maisha ya watu,” alisema Sunkuli, mbunge mteule wa Kilgoris.
Mbunge mteule wa Westlands Tim Wanyonyi alisisitiza kuwa hazina ya maendeleo ya maeneo bunge imehusisha maendeleo nchini ikilinganishwa na kaunti.
Mbunge mteule wa Gatundu Kusini Gabriel Kagombe ambaye anajitosa katika bunge la Agosti kama mbunge kwa mara ya kwanza alikashifu hatua ya mahakama kuu, akisema watapambana kuhakikisha kuwa NGCDF iliyokuwa bado mahakamani inatekelezwa.