Chebor wa UDA ambwaga chini Raymond Moi kunyakua kiti cha mbunge wa Rongai

Mgombea huyo wa chama cha United Democratic Alliance alipata kura 27,021.

Muhtasari

•Moi alikuwa akitafuta muhula wa tatu kwa tikiti ya KANU na alikuwa na matumaini ya kushinda ila akashindwa na Chebor.

•Uchaguzi wa wabunge wa eneo hilo ulifutiliwa mbali mnamo Agosti 9 kwa madai ya kuchanganya karatasi za kupigia kura.

akionyesha cheti chake katika Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Nakuru baada ya kutangazwa mshindi.
Mbunge mteule wa Rongai, Paul Chebor akionyesha cheti chake katika Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Nakuru baada ya kutangazwa mshindi.
Image: LOISE MACHARIA

Paul Chebor almaarufu Mamba ameinuka kutoka kwa mtoto mnyenyekevu wa mkulima mdogo kutoka kijiji cha mbali na kumbwaga chini mtoto wa Rais wa Zamani, marehemu Daniel Moi.

Mgombea huyo wa chama cha United Democratic Alliance alipata kura 27,021 katika uchaguzi ulioahirishwa wa mbunge dhidi ya Raymond Moi aliyemaliza muda wake ambaye alipata kura 14,715.

Mbunge wa zamani wa eneo hilo, Luka Kigen aliibuka wa tatu kwa kura 593.

Moi alikuwa akitafuta muhula wa tatu kwa tikiti ya KANU na alikuwa na matumaini ya kushinda ila akashindwa na Chebor.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mbunge mteule wa Rongai katika Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Nakuru, Chebor aliahidi kufanya kazi na washindani wake ili kuboresha maisha ya wakazi wa Rongai.

Aliwashukuru wapiga kura kwa kumwamini katika nafasi ya uongozi na kuahidi kudumisha amani.

Uchaguzi wa wabunge wa eneo hilo ulifutiliwa mbali mnamo Agosti 9 kwa madai ya kuchanganya karatasi za kupigia kura.

Uchaguzi wa jana ulikumbwa na idadi ndogo ya wapiga kura huku asilimia 5 tu ya waliojiandikisha wakijitokeza kupiga kura.

Rongai ina wapiga kura 84,625 waliojiandikisha.