"Malala hatakuwa kitu chochote Kenya hii" Video ya Atwoli akitamkia laana yaibuka

Kama hakula kweney mikono yangu achaguliwe, kama alikula kwenye mikono yangu asiwe kitu chochote Kenya - Atwoli.

Muhtasari

• “Huyu mtoto anaitwa Malala, mimi ndio nilimpa kiti mwaka 2017. Yule Malala amepotea, na anataja jina langu," - Atwoli.

Uchaguzi wa Kakamega ulikamilika Jumatatu ambapo matokeo yalitolewa Jumanne, ambapo aliyekuwa mkuu wa KETRACO Fernandes Barasa kushinda ugavana kupitia tikiti ya chama cha ODM huku akimbwaga mshindani wake wa karibu Cleophas Malala.

Muda mchache baada ya kutangazwa kwa Barasa kama mrithi wa gavana anayeondoka Wycliffe Oparanya, sasa video ya katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi nchini Francis Atwoli akimlaani Malala kwamba hatakuwa kitu chochote nchini imeibuliwa kwenye mtandao wa Twitter.

Katika video hiyo ya zamani, Atwoli anaonekana akimkashfu Malala huku akijuta kwamba yeye ndiye aliyemuinua seneta huyo anaeondoka wa Kakamega na kumuweka kwenye tasnia ya siasa lakini alikuja akamgeuka na kuingia kweney mrengo wa Ruto ambao Atwoli alikuwa anaupinga na kuukashfu vikali kutokana na tofuait zake za kisiasa na rais mteule William Ruto.

Atwoli anaeleza kwamab katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 yeye ndiye alifadhili kampeni za Malala kuwa seneta ila sasa amemgeuka.

Atwoli anasikika akimtamkia Malala laana na kusema kwamab hawezi kuwa kitu chochote katika nchi hii baada ya kumaliza hatamu yake ya useneta. Video hii imeibuliwa wengi wakianza kusema kwamba laana ya Atwoli ni kama ilimuandama Malala baada ya kupoteza ugavana.

“Huyu mtoto anaitwa Malala, mimi ndio nilimpa kiti mwaka 2017. Yule Malala amepotea, na anataja jina langu, sijakunywa chai kwa nyumba yao, sijakula kwao sijakula kwake. Yeye amekula kwangu, ametumia pesa zangu kuwa seneta. Mimi nasema leo nikiwa nyumbani, hili jua tulipatiwa bure, kama yeye hakukula kwa hii mikono, achaguliwe, kama alikula kwa hii mikono, asiwe kitu chochote katika Kenya hii,” Atwoli anatamka laana kwa Malala.