Ni uchungu kupoteza, Kama hivi ndio Raila amekuwa akihisi mara 5, basi yeye ni shujaa - Malala

Tunamshukuru Raila kwa kuvumilia kupoteza mara 5, sio kitu rahisi - Malala.

Muhtasari

• "Kile tunaomba tu ni kwamba Wakenya wajifunze kukubali matokeo. Najua ni uchungu kupoteza" - Malala.

• Aliibuka wa pili kwa kupata kura 159,508 dhidi ya Fernandes Barasa wa ODM aliyeibuka kidedea kwa kura 192,929.

Aliyekuwa seneta wa Kakamega Cleophas Malala akimkejeli Raila kuwa amekuwa akihisi uchungu kupoteza mara 5
Aliyekuwa seneta wa Kakamega Cleophas Malala akimkejeli Raila kuwa amekuwa akihisi uchungu kupoteza mara 5
Image: Maktaba

Aliyekuwa seneta wa Kakamega Cleophas Malala katika hotuba yake na vyombo vya habari baada ya kupoteza katika kinyang’anyiro cha ugavana Kakamega, ametumia fursa hiyo kutupa kiasi moto kwenye ulimi wa kinara wa muungano wa Azimio One Kenya, Raila Odinga.

Malala alisema kwamba ni wakati sasa Wakenya wajifunze kukubali matokeo na haswa viongozi wale waliokuwa wakiwania na kushindwa.

Katika hotuba hiyo, Malala alisema kwamba yeye amekubali matokeo kikamilifu kwa kushindwa na Fernandes Barasa wa ODM huku akisema kwamba haikuwa rahisi kukubali mpaka kutolea mfano wa Raila kwamba amehisi uchungu wake kama hivyo ndivyo amekuwa akihisi kia baada ya uchaguzi ambao amekuwa akiupoteza kwa mara ya tano sasa katika kipute cha urais.

“Nimekubali matokeo. Sisi hatulalamiki. Hakuna kura iliibiwa Kakamega. Kile tunaomba tu ni kwamba Wakenya wajifunze kukubali matokeo. Najua ni uchungu kupoteza na hata leo nilikuwa nasema kama hivi ndivyo Raila amekuwa akisikia mara tano, ni uchungu sana. Kama hivi ndivyo yeye husikia kila wakati basi ni shujaa kwetu sababu amevumilia mara tano, tunamshukuru kwa kuvumilia, sio kitu rahisi,” Malala anaonekana akisema kwenye klipu moja ambayo ameipakia kweney Twitter yake.

Malala alikuwa akiwania ugavana kwa tikiti ya chama cha ANC kinachoongozwa na mmoja wa vigogo wa muungano wa Kenya Kwanza, Musalia Mudavadi.

Aliibuka wa pili kwa kupata kura 159,508 dhidi ya Fernandes Barasa wa ODM aliyeibuka kidedea kwa kura 192,929.

Uchaguzi huu ulifanyika kuchelewa baada ya kuahirishwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC mnamo Agosti 9 kutokana na mkanganyiko uliotokea wakati wa kusambazwa kwa karatasi za kupiga kura za ugavana.

Sehemu zingine ambazo pia uchaguzi ulioahirishwa ulifanyika ni pamoja na kaunti ya Mombasa katika nyadhifa ya ugavana, eneo bunge la Kacheliba huko West Pokot, Rongai katka kaunti ya Nakuru miongoni mwa sehemu zingine ambazo tayari matokeo yametangazwa na IEBC.