Omtatah asisitiza hakuna yeyote kati ya Ruto na Raila aliyetimiza 50+1

Alisema asilimia ya wapiga kura inavyohesabiwa na IEBC, si sahihi.

Muhtasari

•Anasema kuwa hakuna hata mmoja wa wagombeaji aliyefikia kiwango cha 50+1, ili kutangazwa mshindi.

•"Bila thamani kamili, asilimia haziwezi kutolewa kwa watu binafsi wanaoshiriki uchaguzi," aliambia mahakama.

Mwanaharakati Okiya Omutata katika mahakama ya mombasa Machi 31 2014 ambapo alidai maisha yake yako hatarini baada ya watu wawili wasiojulikana kumkaribia na kumwonyesha bunduki./
Mwanaharakati Okiya Omutata katika mahakama ya mombasa Machi 31 2014 ambapo alidai maisha yake yako hatarini baada ya watu wawili wasiojulikana kumkaribia na kumwonyesha bunduki./
Image: NOBERT ALLAN

Mwanaharakati Okiya Omtatah ameiomba mahakama kufutilia mbali uchaguzi wa urais wa Agosti 9.

Anasema kuwa hakuna hata mmoja wa wagombeaji aliyefikia kiwango cha 50+1, ili kutangazwa mshindi.

Katika wasilisho lake, Omtatah aliambia mahakama ya upeo kuwa suala la kujitokeza kwa wapiga kura halijashughulikiwa ipasavyo na IEBC.

Alisema asilimia ya wapiga kura inavyohesabiwa na IEBC, si sahihi.

“Wapigakura waliojitokeza kupiga kura ni idadi kamili ya jumla ya wapigakura waliojiandikisha kushiriki katika uchaguzi.

"Bila thamani kamili, asilimia haziwezi kutolewa kwa watu binafsi wanaoshiriki uchaguzi," aliambia mahakama.

Seneta huyo mteule wa Busia aliwasilisha zaidi kwamba idadi kamili haiwezi kubadilika kuhusiana na kitu kingine chochote.

Alisema katika ngazi ya kitaifa, rejeleo pekee ambalo mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anaweza kutumia huku akikokotoa asilimia ya waliojitokeza kupiga kura ni sajili ya kitaifa ya wapigakura.

"Ikiwa watu 100 au 1,000 watapiga kura kwa wakati mmoja, watakaojitokeza watakuwa 100 kati ya jumla ya wapiga kura katika rejista ya kitaifa, au 1,000 ya jumla ya wapiga kura katika rejista ya kitaifa," Omtatah alisema.

Alisema wakati mmoja mwenyekiti aliripoti watu 12,065,803 walipiga kura na hii iliwakilisha asilimia 56.17 ya jumla ya wapiga kura 22,120,458.

Hata hivyo, alisema mfanyakazi wa IEBC Moses Sunkuli anatumia idadi sawa ya wapiga kura (12,065,803) kama ilivyoripotiwa na mwenyekiti lakini dhidi ya idadi tofauti ya 21,481,652.

"Huu ni mchezo wa takwimu ambao mahakama hii inakabiliwa nao. Wote wanatoa uwiano sawa wa waliojitokeza kupiga kura wa asilimia 56.17. Nambari sawa ya kiwango tofauti lakini matokeo sawa," Omtatah alisema.

Mapema siku hiyo, wakili Willis Otieno alikashifu IEBC kwa kuruhusu wageni kujipenyeza katika mfumo wao.

Alipuuzilia mbali utetezi wa IEBC kwamba mfumo wao ulikuwa wa uthibitisho akisema kuna ushahidi kinyume.

Otieno zaidi alisema kweli kulikuwa na amani katika Bomas, kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura.

"Ili kuthibitisha kuwa kweli kulikuwa na amani huko Bomas, tulikuwa na kwaya iliyoimba usiku na mchana. Kwaya ni shahidi wangu," alisema.

Wakili huyo pia aliwasilisha kwamba kuhusu suala la mawakala, mpiga kura wa kawaida wa Kenya hawezi kuwa na mawakala 46,000 kutazama uchaguzi.

Alisema wajibu ni kwa IEBC kuandaa uchaguzi huru na wa haki.

Vyama hivyo pia viliiomba mahakama kumfungulia mashtaka Chebukati kwa makosa ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu uliopita.

"Mahakama haipaswi kuogopa ikiwa itaona ni muhimu kumfungulia mashtaka Chebukati kwa makosa na njia ya pekee ambayo alishughulikia uchaguzi, na kuwadhuru Wakenya," mahakama ya upeo ilisikiza.