- Kisang alisherehekea matokeo ingawa wapinzani wake walikataa matokeo hayo kwa madai kuwa kulikuwa na dosari kubwa
Aliyekuwa mbunge wa Marakwet Magharibi, William Kisang, aliwashinda wagombea wengine 20 wa kiti cha mchujo wa UDA katika mchujo wa useneta wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Huku UDA kikiwa chama kikuu zaidi katika eneo hili, Kisang anachangamoto ya kuchaguliwa kuwa Seneta mnamo Januari 5 2023 kupitia uchaguzi.
Uchaguzi huo ulitokana na kujiuzulu kwa Waziri wa Barabara Kipchumba Murkomen ambaye alikuwa amechaguliwa Agosti 9 lakini akajiuzulu baada ya kuteuliwa na Rais William Ruto.
Katika kura za mchujo za UDA Jumamosi Kisang alipata kura 28,126 mbele ya wapinzani wake Tim Kipchumba na Jonah Tanui aliyepata kura 26,756 na 26,735 mtawalia.
Kisang alisherehekea matokeo ingawa wapinzani wake walikataa matokeo hayo kwa madai kuwa kulikuwa na dosari kubwa.
“Namshukuru Mungu kwa ushindi huo na nina furaha kwamba mapenzi ya wananchi yamekuwepo,” alisema Kisang.
Nicodemus Bore ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi alitangaza Kisang kuwa mshindi na kupewa cheti cha chama.
Kisang ambaye alihudumu kama mbunge kwa mihula miwili huko Marakwet Magharibi ameshindwa katika uchaguzi wa Agosti lakini akasema anashukuru Mungu amemfungulia mlango mwingine.
"Ninaahidi kuwatumikia watu wetu kwa kujitolea na maono makubwa kwa kaunti yetu", alisema.