Gachagua kushuhudia kuapishwa kwa Kahiga Kama Gavana wa Nyeri

Gachichio alisema kamati hiyo imetenga Sh5 milioni kwa hafla hiyo.

Muhtasari

•Gachagua ni miongoni mwa wageni zaidi ya 4,000 wanaotarajiwa kuhudhuria hafla ya Alhamisi ya kuapishwa kwa Mutahi Kahiga kama gavana wa tano wa Nyeri.

 

RIGATHI GACHAGUA
Image: WLFRED NYANGARESI

Naibu Rais mteule, Rigathi Gachagua ni miongoni mwa wageni zaidi ya 4,000 wanaotarajiwa kuhudhuria hafla ya Alhamisi ya kuapishwa kwa Mutahi Kahiga kama gavana wa tano wa Nyeri.

Hafla hiyo inatazamiwa kufanyika katika uwanja mpya wa mabasi ya Nyeri uliojengwa katika eneo la 'Asian Quarters' katika mji wa Nyeri.

Wageni na wananchi wanatarajiwa kuketi kabla ya saa tatu asubuhi huku uapisho ukianza saa nne  asubuhi na kuongozwa na Jaji James Wakiaga wa mahakama kuu ya Murang’a.

Akihutubia wanahabari katika kituo cha mabasi cha kisasa kilichogharimu Sh600 milioni, baada ya kukagua maandalizi yanayoendelea, mwenyekiti wa kamati hiyo Benjamin Gachichio alisema kamati hiyo imetenga Sh5 milioni kwa hafla hiyo.

Gachichio alisema kuwa kamati hiyo itatuma zaidi ya mabasi 40 kuwasafirisha wananchi kutoka wadi zote 30 za kaunti hiyo.

“Hii ni mchakato wa kisheria ambayo lazima ufanywe kuligana na sheria. Mipango yote imefanywa, tumewaalika wawakilishi kutoka sehemu zote za kaunti kuhakikisha kuwa kaunti inawakilishwa vyema. Tumewakodishia mabasi tutawasafirisha na kuwarudisha," alisema Gachichio.

"Suala la mpangilio wa usalama limeshughulikiwa, hakuna timu ambayo haijahusishwa na mchakato huu, kutoka kwa serikali ya kitaifa; idara ya mahakama, polisi, kamishna wa kaunti na Wizara ya ugatuzi wako hapa kutuongoza,” aliongeza Gachichio.

Gavana mteule wa Nyeri, Mutahi Kahiga, alihifadhi wadhifa wake wa ugavana baada ya kupata kura 213,373 katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.