"Hata kuiba kunahitaji akili!" Ngunjiri Wambugu alalamikia wizi wa kura Nyeri

Mbunge huyo anayeondoka ametilia shaka idadi ya wapiga kura walioripotiwa kujitokeza mnamo siku ya uchaguzi.

Muhtasari

β€’Ngunjiri amepinga matokeo yaliyotolewa Alhamisi huku akitilia shaka idadi ya wapiga kura walioripotiwa kujitokeza siku ya Jumanne.

β€’Ngunjiri alidokeza kuwa kutakuwa na marudio ya uchaguzi katika siku zijazo na kuwashauri watu kutotupa nguo zao za kampeni.

Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu akiwahutubia waandishi wa habari
Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu akiwahutubia waandishi wa habari
Image: MAKTABA

Mbunge wa Nyeri anayeondoka Ngunjiri Wambugu ameeleza kutoridhishwa kwake na mchakato wa uchaguzi katika eneo bunge lake.

IEBC ilimtangaza Duncan Maina Mathenge kama mbunge mteule wa Nyeri Town baada ya kuzoa kura 41, 007  dhidi ya 11,808 za Ngunjiri.

Mbunge huyo wa muhula mmoja amepinga matokeo yaliyotolewa Alhamisi huku akitilia shaka idadi  ya wapiga kura walioripotiwa kujitokeza siku ya Jumanne.

"Kwa hivyo  Nyeri Town ilikuwa na karibu asilimia 70 ya wapiga kura waliojitokeza? Kweli? πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚πŸ˜‚ Hata kuiba kunahitaji akili, watu wema. Machozi mengi yamo njiani … πŸ˜‰" Ngunjiri alisema kupitia Facebook.

Aliongeza, "Kwa hivyo, watu 56,039 walimpigia kura mbunge Jumanne katika Nyeri Town. Jumla ya wapiga kura waliojiandikisha ni 89,000. Kwa hivyo mnamo Jumanne tulikuwa na wapiga kura 64.3% katika Mji wa Nyeri πŸ˜‡πŸ˜‰."

Mgombea huyo wa Jubilee pia alitilia shaka idadi ya wapiga kura walioripotiwa kujitokeza katika eneo bunge la Kieni jirani.

Alidokeza kuwa atakuwa akielekea mahakamani kupinga matokeo ya ubunge yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi.

"Watu watulie - waweke pressure zero. Malalamishi ni sehemu ya uchaguzi. Ikiwa umeshinda halali, ni rahisi kudhibitisha. Unapaswa kuwa na wasiwasi ikiwa tu uliongeza idadi fulani ya kura kwa kila kituo cha kupigia kura πŸ˜‰,"

Pia alidokeza kuwa kutakuwa na marudio ya uchaguzi katika siku zijazo na kuwashauri watu kutotupa nguo zao za kampeni.

Kanini Kega ambaye amehudumu kama mbunge wa Kieni kwa mihula miwili pia alibwagwa chini na Njoroge Wainaina wa UDA.

UDA imeshinda viti vyote sita vya ubunge kaunti ya Nyeri.