IEBC kutangaza matokeo ya urais leo Jumatatu saa tisa alasiri

Uhakiki wa fomu za matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 ulikamilika Jumatatu asubuhi.

Muhtasari

•Tume ya IEBC ilisema kwamba itatangaza matokeo ya kura ya urais ya Agosti 9 mwendo wa saa tisa mchana.

•Chebukati anatarajiwa kumtangaza rais mpya wa Kenya baada ya shughuli ya uhakiki wa fomu za matokeo ya urais  na ujumuishaji wa kura  kukamilika.

akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Image: ENOS TECHE

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC)  imesema itatangaza matokeo ya uchaguzi wa urais hivi leo.

Katika barua ya mwaliko wa vyombo vya habari iliyotolewa Jumatatu, tume hiyo ilisema kwamba itatangaza matokeo ya kura ya urais ya Agosti 9 mwendo wa saa tisa mchana.

"Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inakualika kuangazia tangazo la Matokeo ya Urais mnamo Jumatatu Agosti 15, 2022 katika Bomas of Kenta saa tisa alasiri," Barua ya IEBC ilisoma.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anatarajiwa kumtangaza rais mpya wa Kenya baada ya shughuli ya uhakiki wa fomu za matokeo ya urais kutoka maeneobunge yote na ujumuishaji wa kura  kukamilika.

Uhakiki wa fomu za matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9  ulikamilika Jumatatu asubuhi baada ya kuendelezwa kwa siku tano.

Meza 15 za kufanyia uhakiki wa matokeo katika Bomas of Kenya zilikuwa tupu  kufikia Jumatatu asubuhi.

Meza chache tu zilikuwa na makarani wa IEBC ambao walikuwa wanashiriki katika mazungumzo ya sauti ya chini baada ya kumaliza kazi za karatasi.

Ndani ya ukumbi wa Bomas, viti vya Azimio na Kenya Kwanza vilikuwa vimekaliwa kufikia saa tatu asubuhi.

Wajumbe na mabalozi wa kigeni pia waliketi mapema saa mbili unusu asubuhi kuashiria matangazo yanawezekana kutolewa leo.

Pia kuna uwepo mkubwa wa wanausalama katika ukumbi wa mikutano, maeneo jirani na lango kuu.

Mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio iko ukumbini zikingoja tangazo kubwa la mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati