Jeki kwa Raila huku Mwangi wa Iria akijiunga na Azimio-One Kenya

Wa-Iria alieleza kuwa amechukua hatua hiyo baada ya Raila kukubali kuzingatia manifesto yake.

Muhtasari

•Mwangi wa Iria alieleza kuwa amechukua hatua hiyo baada ya Raila kukubali kuzingati manifesto yake.

•Wa Iria aliwasihi wapiga kura wa kaunti yake ya Murang'a kuwa nyuma yake anapojiunga na Azimio.

akiwahutubia waandishi wa habari
Gavana wa Muranga Mwangi wa Iria akiwahutubia waandishi wa habari
Image: EZEKIEL AMINGA

Kiongozi  chama cha  Usawa kwa Wote Mwangi wa Iria amejiunga na muungano wa Azimio la Umoja- One Kenya.

Akihutubia waandishi wa habari Jumanne, Mwangi alieleza kuwa amechukua hatua hiyo baada ya Raila kukubali kuzingatia manifesto yake.

Gavana huyo wa Murang'a alisema kuwa alishiriki kikao cha pamoja na Raila baada ya IEBC kumzuilia kuwania urais ambapo aliwasilisha manifesto zake zote, wakajadiliana na kukubali kufanya kazi pamoja.

"Kupitia manifesto ya pamoja, chama cha usawa kwa wote kiliamua kuunga mkono azma ya Raila Odinga na wafuasi wangu watakuwa nyuma ya Raila Odinga," Mwangi alisema katika mkutano na waandishi wa habari katika hoteli ya Serena, Nairobi.

Gavana huyo wa  muhula wa pili alibainisha kuwa Raila alikubali kutekeleza mpango wake wa 'Ngombe moja, boma moja' na kuimarisha ukulima  na biashara katika kaunti ya Murang'a.

Wa Iria aliwasihi wapiga kura wa kaunti yake ya Murang'a kuwa nyuma yake anapojiunga na Azimio huku akiwaahidi kudai wadhfa katika serikali ya Raila ikiwa atachaguliwa kuwa rais.

"Ningependa watu wa Murang'a muwe nyuma yangu. Mimi ni kiongozi wenu. Wacha kura zote 620,000 ziende kwa Raila. Tutaagiza Raila anipatie wadhfa wa waziri.Mimi na Martha na Peter Munya akiwa amekaa upande ule mwingine tutaendeleza mlima huu," Wa Iria alisema.

Gavana huyo aliwakashifu vigogo wengine wa siasa katika Mlima Kenya ambao wanadai kuwa wanawakilisha eneo hilo lote huku akisisitiza kuwa yeye ndiye kiongozi halisi wa Murang'a.