Kindiki Kithure afunguka sababu za kutohudhuria uzinduzi wa Gachagua

Muhtasari

•Muungano wa Kenya Kwanza ulimchagua mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua kuwa mgombea mwenza wa Ruto.

•Siku moja baadaye, Jumatatu, Kindiki alitangaza kustaafu kutoka kwa siasa za kuchaguliwa kuanzia Agosti 10.

Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki
Image: Andrew Kasuku

Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki ameeleza ni kwa nini hakuwepo wakati wa kutambulishwa kwa mgombea mwenza wa Naibu Rais William Ruto Jumapili katika mtaa wa Karen.

Muungano wa Kenya Kwanza ulimchagua mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua kuwa mgombea mwenza wa Ruto. Kindiki ni miongoni mwa waliopendekezwa zaidi kuchukua wadhifa huo.

Siku ya Jumatano, Kindiki alisema alikosa hafla hiyo kwa sababu ya ilitokea wakati usiofaa na kutokuwepo kwa mawasiliano mwafaka.

Katika mahojiano katika runinga ya Citizen, Kindiki alifichua kuwa mkutano wa kubaini ni nani angekuwa mgombea mwenza bora wa Ruto ulikamilika mwendo wa saa sita usiku, na akaondoka nyumbani kwa Naibu Rais mwendo wa saa nne asubuhi ya  Jumapili.

"Asubuhi, nilienda kwenye sehemu yangu ya kawaida ya kuabudia, na nadhani DP alienda katika kanisa iliyo ndani ya makazi yake. Lakini ibada katika kanisa yangu  ilichelewa kidogo."

Seneta huyo alieleza kuwa baadhi ya wenzake waliokuwepo wakati wa uzinduzi huo walimfahamisha, na mara moja akaondoka kanisani.

"Niliona missed call kutoka kwa kiongozi wa chama changu, nikampigia tena, lakini hakupokea... nilijua kuwa uamuzi ulikuwa umetangazwa," alisema na kuongeza kuwa hangeweza kufika kwenye makazi ya Ruto kwa wakati.

Baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya walikuwa wamempendeza Kindiki kuwa mgombea mwenza wa  Kenya Kwanza, lakini baada ya mkutano wa saa masaa 17, uongozi ukaamua kumkabidhi Gachagua wadhifa huo.

Siku moja baadaye, Jumatatu, Kindiki alitangaza kustaafu kutoka kwa siasa za kuchaguliwa kuanzia Agosti 10.

Alisema hatapatikana kuteuliwa katika nafasi yoyote  lakini akaahidi kumfanyia kampeni Ruto na timu ya Kenya Kwanza.

"Jaribio langu likiwa limefeli, nimechukua uamuzi wa kupumzika kutoka kwa siasa za uchaguzi kuanzia Agosti 10," alisema.

"Nitatumia muda wa mapumziko kujipanga upya huku nikiunga mkono chama changu cha UDA na Kenya Kwanza kuhakikisha wanatumikia Wakenya pindi wanapoingia madarakani."

Akimzindua Gachagua, Ruto alisema timu yake iliamua kumteua kwa sababu yeye ni mdadisi mahiri, ana kanuni thabiti na ni hana woga.

"Gachagua ni rafiki yangu ambaye nimefanya naye kazi, haswa kwenye mtindo huo wa Bottom-Up Economic na tulianza safari hiyo pamoja. Anaelewa masuala ya watu, ana shauku na watu wa kawaida," Ruto alisema.