Mamake Ruto awasili Bomas kufuatilia matangazo ya matokeo ya urais moja kwa moja

Bi Sarah Cheruiyot aliwasili Jumatatu alasiri akiwa ameandamana na wanafamilia wengine.

Muhtasari

•Bi Cheruiyot  amewasili katika ukumbi wa Bomas Of Kenya kabla ya tume ya uchaguzi na mipaka nchini kutangaza matokeo ya urais.

Mamake DP Ruto, Sarah Cheruiyot, wanafamilia wengine katika Bomas Of Kenya
Mamake DP Ruto, Sarah Cheruiyot, wanafamilia wengine katika Bomas Of Kenya
Image: HISANI

Mamake Naibu Rais William Ruto amewasili katika ukumbi wa Bomas Of Kenya kabla ya tume ya uchaguzi na mipaka nchini kutangaza matokeo ya urais

 Bi Sarah Cheruiyot aliwasili Jumatatu alasiri akiwa ameandamana na wanafamilia wengine. Alikuwa amevalia nguo nyeupe na kofia kichwani alipowasili.

Mama Sarah sasa anaungana na mwanawe Ruto na mkaza mwanawe Rachel Ruto ambao walifika ukumbini mwendo wa saa tisa kasorobo.

Kundi kubwa la wanasiasa na washika dau wengine tayari wamewasili katika ukumbi wa Bomas ili kufuatilia matangazo ya matokeo ya urais.

Chebukati anatarajiwa kumtangaza rais mpya wa Kenya baada ya shughuli ya uhakiki wa fomu za matokeo ya urais kutoka maeneobunge yote na ujumuishaji wa kura  kukamilika.

Uhakiki wa fomu za matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9  ulikamilika Jumatatu asubuhi baada ya kuendelezwa kwa siku tano.

Hapo awali, kiongozi wa Roots Party George Wajackoyah na David Mwaure wa Agano walifika katika ukumbi wa Bomas of Kenya kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo.