MC Jessy ajiondoa kwenye kinyang'anyiro cha ubunge Imenti Kusini, apewa kazi na Ruto

Muhtasari

•Ruto amesema Jessy atajiunga na timu  ya kampeni zake za urais baada ya kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Mgombeaji ubunge Imenti Kusini Mwiti Kathaara, Naibu Rais William Ruto na MC Jessy
Mgombeaji ubunge Imenti Kusini Mwiti Kathaara, Naibu Rais William Ruto na MC Jessy
Image: TWITTER// RUTO

Mchekeshaji Jasper Muthomi almaarufu MC Jessy amesitisha azma yake ya kuwania ubunge wa Imenti Kusini.

Naibu rais William Ruto amesema Jessy atajiunga na timu  ya kampeni zake za urais baada ya kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Jessy amemwachia nafasi Mwiti Kathara kupeperusha bendera ya UDA katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.

"MC Jessy (Jasper Muthomi) sasa atajiunga na timu ya kampeni za urais baada ya kuahirisha azma yake ya kuwania ubunge wa Imenti Kusini kwa upendeleo wa Mwiti Kathaara," Ruto ametangaza kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mwezi Januari, mchekeshaji  huyo alithibitisha kuwa amejiunga rasmi na chama cha UDA baada ya kushiriki mashauriano mapana na washika dau.

Jessy alisema Ruto alimpigia simu na kumwalika kwenye chama cha UDA.

"Sasa ni wazi maono yanaelekea wapi. Baada ya siku nyingi za mikutano ya mashauriano na watu wangu wa Imenti Kusini, nimealikwa rasmi kujiunga na UDA," alisema.

Aliongeza kuwa alikubali kujiunga na UDA kwa sababu huko ndiko watu wake walitaka awe mwanachama.