Mgombea urais Peter Gichira ajiondoa kwenye kinyang'anyiro kwa madai ya kutekwa nyara

Muhtasari

•Peter Gichira aliingia katika kituo cha polisi cha Lungalunga akidai kuwa alitekwa nyara siku mbili zilizokuwa zimepita.

•Gichira aliambia mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anatazamia uchunguzi wa kina utafanyika  kuhusu kisa hicho .

Mwaniaji huru wa urais Solomon Gichira (kushoto) na mgombea mwenza wake Watimah Kelly katika mahakama ya Milimani, Juni 16, 2017.
Mwaniaji huru wa urais Solomon Gichira (kushoto) na mgombea mwenza wake Watimah Kelly katika mahakama ya Milimani, Juni 16, 2017.
Image: COLLINS KWEYU

Mgombea urais Peter Solomon Gichira amejiondoa katika kinyang'anyiro hicho kwa  madai kuwa alitekwa nyara na watu wasiojulikana ambao walimyang’anya  mali  za thamani katika eneo la Viwandani Nairobi.

Peter Solomon Gichira almaarufu Ptah Solomuz Gichira mnamo Mei 25, aliingia katika kituo cha polisi cha Lungalunga akidai kuwa alitekwa nyara siku mbili zilizokuwa zimepita.

Gichira alisema kuwa alitekwa nyara alipokuwa akielekea Bomas of Kenya kwa mkutano wa kabla ya uteuzi ambao uliandaliwa naTume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mgombea urais huru huyo ameiandikia IEBC barua akisema hatawania kiti hicho  kama ilivyokuwa amepanga hapo awali.

“Kwa hivyo, ninasitisha kugombea nafasi ya kuchaguliwa ya Rais wa Jamhuri ya Kenya. Naomba niwatakie nyinyi - wafanyikazi wa IEBC na wagombeaji wote - uchaguzi mwema na wenye mafanikio,” Gichira alisema kwenye barua hiyo.

Polisi walithibitisha kuwa Gichira aliripoti kisa hicho kituoni.

Katika barua hiyo ya Mei 25, Gichira alisema alitekwa nyara na watu wasiojulikana mnamo Mei 23 mwendo wa saa mbili unusu asubuhi, kabla ya kupatikana baadaye akiwa ametupwa kando ya barabara ya Lungalunga jijini Nairobi.

“Katika harakati hizo, nilipoteza fomu zangu zote nilizosaini kwa ajili ya kuunga mkono ugombea wangu; Nakala za Vitambulisho vya Kitaifa ambazo nilikuwa nimekusanya ili kuunga mkono sahihi; diski kuu ya nje na kompyuta ndogo zote zikiwa na data ya kielektroniki ya fomu zilizotiwa saini, na simu yangu na kadi ya kitambulisho.”

Hii ilitokea alipokuwa akisubiri teksi katika eneo la Tena, kando ya Barabara ya Outer Ring.

Alisema gari lilisimama karibu yake na mmoja wa watu watatu waliokuwamo akamtaja kwa jina na alipoangalia kutambua ni kina nani wakamsukuma ndani na kumwamuru afungue simu yake ya mkononi.

Kisha watu hao walimpokonya vitu vyake vya thamani kabla ya kumnyunyizia kemikali isiyojulikana iliyomfanya alale hadi siku iliyofuata Mei 24 mwendo wa saa 6 asubuhi.

Aliwaambia polisi msamaria mwema alimpeleka hospitali na kumsaidia kwa simu ya mkononi kumpigia mkewe na baadaye kwenda kuripoti mater.

Gichira aliambia mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anatazamia uchunguzi wa kina utafanyika  kuhusu kisa hicho .

"Nimejaribu kutoa maelezo haya ya kutekwa kwangu ili mfikirie kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Jeshi la Polisi nchini, katika kuimarisha usalama wa wagombea na wa Uchaguzi Mkuu."

Gichira alisema baada ya kuzingatia muda, juhudi na rasilimali za kifedha zilizohusika katika zoezi jipya la kukusanya saini, muda ambao IEBC inao kwa stakabadhi hizo na kiwewe alichokuwa amekumbana nacho alipata kuwania kwake hakufai tena.

Polisi wanaoshughulikia suala hilo walisema wanapanga kutembelea maeneo ambayo alisema tukio hilo lilitokea ili kudhibitisha hilo.

Hii ilikuwa baada ya IEBC kumwambia hataruhusiwa kuwasilisha karatasi zake na kuwania kama mgombeaji huru wa kiti cha urais.

Baadaye aliachiliwa kwa shtaka la kujaribu kujiua na uharibifu mbaya wa mali.

Hakimu Mkuu Francis Andayi, hata hivyo, alimtia hatiani kwa shtaka la kuleta fujo katika afisi za IEBC.

Mahakama ilimwachilia Gichira, lakini ikaonya kutotenda kosa lingine lolote katika muda wa miezi sita iliyofuata.