Mkanganyiko Roots Party huku Wajackoyah akimuidhinisha Raila na Wamae akimpendelea Ruto

Justina alisema endapo itatokea haja ya wao kuidhinisha mpinzani wao yeyote, atamuunga mkono Ruto.

Muhtasari

•Justina alisema ni kweli mgombea urai wao anamuunga mkono Raila na kubainisha kuwa hakuombwa ushauri wowote.

•Wajackoyah alipuuzilia mbali madai hayo na kusisitiza kuwa mgombea wao atakuwa kwenye debe mnamo Agosti 9.

Mgombea Urais wa Roots Party George Wajackoyah na mgombea mwenza wake Justina Wamae.
Mgombea Urais wa Roots Party George Wajackoyah na mgombea mwenza wake Justina Wamae.
Image: EZEKIEL AMINGA

Siku ya Jumatano tetesi kuwa  mgombea urais wa Roots Party George Wajackoyah amemuidhinisha kinara wa ODM Raila Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya ziliibuka na kuenezwa kote mitandaoni.

Tetesi hizo ziliungwa mkono na klipu  ndogo ya video iliyomuonyesha Wajackoyah akimtambua  Raila kama mkombozi wa Kenya.

Video hiyo ilimuonyesha kiongozi wa Roots Party akimpa sifa  Raila kwa kuhamasisha safari yake ya kuwa  mkombozi.

"Niko hapa kujiunga na kundi la wakombozi katika nchi hii. Mtu ninayemtazama, anayenifanya nisimame hapa si mwingine bali ni Raila Amollo Odinga," Wajackoyah anadaiwa kusema.

Chama cha Roots hata hivyo kilijitokeza kupuuzilia mbali madai hayo na kusisitiza kuwa mgombea wao atakuwa kwenye debe mnamo Agosti 9.

Kupitia msemaji wake Wlison Muirani almaarufu Jaymo ule Msee, chama cha Roots  kilidai kuwa video iliyokuwa ikisambazwa mitandao ilikuwa imefanyiwa ukarabati.

"Tungependa kueleza kinaga ubaga kuwa tuna mgombea urais ambaye yuko kwenye debe na atashinda uchaguzi huu. Hatujaidhinisha mgombea mwingine yeyote!" Taarifa iliyotolewa na Roots Party Jumatano asubuhi ilisoma.

Chama hicho kilibainisha kuwa baadhi ya washindani wao wamezamia kwenye mbinu mbaya baada ya kupatwa na wasiwasi kuhusu matokeo ya uchaguzi  huku kikiwahakikishia wafuasi wao kuhusu ushindi katika kinyang'anyiro cha wiki ijayo

Hata hivyo, baadae siku hiyo mgombea mwenza wa urais wa chama hicho Justina Wamae alijitokeza na kuunga mkono madai kuwa Wajackoyah anampendelea mgombea wa Azimio la Umoja Raila Odinga.

Justina alisema kuwa ni kweli mgombea urai wao anamuunga mkono Raila na kuweka wazi kuwa hakuombwa ushauri wowote kuhusiana na hatua hiyo.

"Ni kweli madai kwamba mkuu wangu na kiongozi wa chama anaunga mkono Azimio. Lakini hatujajadili hilo kama Chama, hatujakubaliana na wala sijashauriwa," Justina aliambia runinga ya Citizen.

Justina hata hivyo alibainisha kuwa endapo itatokea haja ya wao kuidhinisha mpinzani wao yeyote, basi atamuunga mkono William Ruto wa UDA.

Alisema kufikia Jumatano, viongozi wa chama wanaendeleza kampeni zao na kuuza sera za chama kwa wananchi.

Matukio hayo mapya yanaonekana kuzua hali ya sintofahamu katika chama ambacho kinashiriki uchaguzi wa rais kwa mara ya kwanza