Raila aongoza zaidi kwa umaarufu dhidi ya Ruto, Wajackoyah ainuka kwa kishindo- Kura ya Maoni

Muhtasari

•Raila ameendelea kuongoza zaidi huku 44.6% ya wapiga kura wakisema kuwa ndiye mgombea urais wanayempendelea ikilinganishwa na  38.9% ya Ruto.

•Chaguo la Martha linaonekana kumsaidia Raila katika uchaguzi huo huku Rigathi akionekana kutomtia nguvu Ruto.

Naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga
Naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga
Image: STAR

Mgombea urais wa Azimio- One Kenya Raila Odinga ameendelea kuongoza zaidi katika kinyang'anyiro cha urais huku asilimia 44.6 ya wapiga kura wakisema kuwa ndiye mgombea urais wanayempendelea ikilinganishwa na asilimia 38.9 ya DP William Ruto, kwa mujibu wa kura ya maoni ya hivi punde ya Radio Africa.

Uongozi huu wa 5.7%  uko juu ya asilimia ya makosa ya kura ya maoni. Ni mabadiliko makubwa kwa Raila ambaye mnamo Julai 2021 alikuwa na asilimia 14 pekee ya uungwaji mkono, kulingana na kura za maoni za Radio Africa, ikilinganishwa na asilimia 42 za Ruto kwa wakati huo..

Ikiwa uchaguzi wa urais ungefanyika mwaka mmoja uliopita, William Ruto angeweza kuwa mshindi wa wazi.

Sasa kinadharia inawezekana kwamba Raila anaweza kushinda katika duru ya kwanza, ikizingatiwa pia wapiga kura ambao hawajaamua na wale wanaosema hawatapiga kura kabisa.

Kulingana na kura ya maoni, 74.8% ya waliohojiwa bila shaka watapiga kura na 18.9%  pengine watapiga kura, ambayo ni jumla ya asilimia 93.7. Asilimia nyingine 3.2 walisema pengine hawatapiga kura na asilimia 3.1 walisema bila shaka hawatapiga kura.

Wale amabo hawajaamua (asilimia 8.7) wanaegemea zaidi kwa Raila (46.5%) huku 40.6  wakiegemea upande wa DP Ruto.

Iwapo wapiga kura ambao hawajaamua watagawanyika kwa njia sawa kati ya Ruto na Raila, na asilimia sita wasipige kura, Raila anaweza kupita kura nyingi na asilimia 51.5 katika duru ya kwanza ikiwa nia ya kupiga kura haitabadilika.

Radio Africa ilifanya kura yake kupitia njia ya SMS mnamo Juni 8 na 9 ikiwa na asilimia 1.5 ya makosa kutoka kwa wahojiwa 4,780 kutoka kaunti zote 47.

Wiki mbili zilizopita, Raila alimchagua mwanaharakati mkongwe na mwanasiasa Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake huku Ruto akimchagua mbunge wa Mathira na mhamasishaji wa Central Kenya Rigathi Gachagua kuwa mgombea mwenza wake.

Chaguo la Martha linaonekana kumsaidia Raila katika uchaguzi huo huku Rigathi akionekana kutomtia nguvu Ruto.

Prof George Wajackoyah ameonekana kuwashawishi wapiga kura vizuri na ahadi yake ya kuhalalisha bangi. Kura ya maoni ya Radio Africa iligundua kuwa aliungwa mkono na asilimia 2.7 ya waliohojiwa kitaifa, akiwa mgombea pekee mbali na Raila na Ruto aliyepita zaidi ya asilimia 1.0.

Kwa mara ya kwanza, uongozi wa Ruto katika eneo la Kati umeshuka chini ya nusu, hadi asilimia 49.4, huku Raila akiwa asilimia 20.9. Kipengele cha ushawishi kinaweza kuwa kuingia kwa Wajackoyah ambaye alipata uungwaji mkono wa 3.9%.

Ruto na Raila kila mmoja anaongoza katika mikoa mitano.

Ruto pia anaongoza katika North Rift akiwa na 56.0% ikilinganishwa na Raila 31.3%; katika South Rift akiwa na 49.7 ikilinganishwa na Raila 39.9%; katika Kaskazini Mashariki akiwa na 45.2% dhidi ya 39.7% ya Raila; na Mashariki ya Juu na 54.1% ikilinganishwa na 34.5% ya Raila.

Raila anaongoza Nairobi kwa uungwaji mkono wa 52.2%  ikilinganishwa na 29.1%  ya Ruto; Pwani anaongoza na 49.2%  dhidi ya 34.4% za Ruto; katika Lower Eastern anaongoza na 54.3%  dhidi ya 27.4 ya Ruto;Nyanza na 66.8%  dhidi ya 19.9% za Ruto; na eneo la Magharibi kwa 50.9% dhidi ya 33.2 za Ruto.

Katika eneo la Lower Eastern, kurejea kwa Kalonzo Musyoka kunaonekana kuzidisha umaarufu wa Raila katika Ukambani.

Katika eneo la Magharibi, Raila amepata kura nyingi kwa mara ya kwanza.Jambo lingine muhimu linaonekana kuwa Raila anaingia kwenye kura za vijana.

Kura ya maoni ya Radio Africa iligundua kuwa Raila aliungwa mkono na asilimia 43.5 ya waliohojiwa wenye umri wa miaka 18-29 ikilinganishwa na asilimia 38.4 ya Ruto. Raila pia anaongoza na idadi ya watu wazee.

Prof Wajackoyah ana uungwaji mkubwa wa 3.5%  kati ya vijana wenye umri wa miaka 18-29.Ruto anaungwa mkono na wanawake zaidi kwa asilimia 39.7 ikilinganishwa na asilimia 38.9 ambao wanamuunga mkono Raila.

Raila anaongoza akiwa na wanaume wanaomuunga mkono kwa asilimia 49.6 hadi 38.2 kwa Ruto.

Gharama ya Juu ya Maisha ilitajwa na asilimia 57.1 ya waliohojiwa kama jambo linalowatia wasiwasi zaidi; rushwa kwa asilimia 15.8; na ukosefu wa ajira kwa asilimia 15.0. Masuala mengine hayakuwa katika na takwimu kubwa.

Ruto na Raila waliungwa mkono kimsingi kwa 'Ubora wa Uongozi' na asilimia 28.9 na 36.3 ya waliohojiwa mtawalia.

Hata hivyo sababu kubwa iliyofuata kwa Raila ilikuwa 'Mipango ya Nchi'. (asilimia 20.0) na 'Anajali Watu Kama Mimi' kwa Ruto (asilimia 21.0).

Jambo la tatu kwa Raila ni 'Mwaminifu na Mwaminifu' (asilimia 10.0) na 'Mipango ya Nchi' (asilimia 18.2) ya Ruto.

(Utafsiri: Samuel Maina)