Raila na Sakaja watamba kwa umaarufu Nairobi- Kura ya maoni

Muhtasari

•Raila na mgombea mwenza Martha Karua waliidhinishwa na asilimia 49 ya wapiga kura waliohojiwa.

•Naibu rais William Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua waliidhinishwa na 30% ya wahojiwa.

Mgombea urais Raila Odinga na Mgombea ugavana wa Nairobi Johnson Sakaja
Image: HISANI

Mgombea urais wa Azimio-One Kenya ndiye anayependekezwa zaidi katika Kaunti ya Nairobi ikiwa uchaguzi ungefanyika leo, kura ya maoni ya Infotrak inaonyesha.

Utafiti huo ulisema Raila na mgombea mwenza Martha Karua waliidhinishwa na asilimia 49 ya wapiga kura waliohojiwa.

Mpinzani wake wa karibu, DP William Ruto na mgombea mwenza Rigathi Gachagua waliidhinishwa na 30%.

Wagombea wa chama cha Roots George Wajackoyah na Justina Wamae waliidhinishwa kwa 5% huku David Waihiga wa Agano na Ruth Mutua wakipata asilimia 0.3.

Asilimia 15 ya waliohojiwa walikataa kutaja  wanamuunga mkono mgombea urais yupi katika uchaguzi wa Agosti 9.

Kwa upande wa ugavana, 39% ya wahojiwa walimpendekeza seneta Johnson Sakaja kuchukua wadhifa huo. Sakaja anawania kiti hicho kwa tikiti ya chama cha UDA kilicho chini ya mwavuli wa Kenya Kwanza.

Polycarp Igathe ambaye anawania kiti hicho kwa tikiti ya Jubilee alifuata kwa karibu huku akifurahia uungwaji mkono wa asilimia 33%.

Asilimia 0.4 pekee ya wahojiwa walisema wangempigia kura mgombea ugavana huru Agnes Kagure.

24% ya wahojiwa hata hivyo bado hawajafanya maamuzi yao katika wadhifa huo, kwa mujibu wa kura hiyo ya maoni.

Edwin Sifuna wa ODM anaongoza kwa umaarufu katika wadhifa wa useneta, kura ya maoni ya Infotrak imeashiria.

Sifuna anaungwa mkono na asilimia 44 ya waliohojiwa huku Margret  Wanjiru wa UDA ikifuata kwa asilimia 12.

Asilimia 1 ya waliohojiwa wanaunga mkono wagombea useneti wengine huku asilimia  39 wakiwa hawajafanya maamuzi yao. 5% walikataa kujibu.

Utafiti huo uliofadhiliwa na Infotrak ulifanyika kati ya Julai 2-3 kupitia mahojiano ya simu ya Kompyuta.

Kura hiyo ya maoni ilikuwa na asilimia ya makosa ya ±3.

Jumla ya wakazi 1024 walihojiwa kutoka majimbo yote 17 ya uchaguzi na kata 85.