Ruto hatimaye awasiliana na rais Uhuru baada ya miezi

Wawili hao pia waliweza kujadili mchakato wa mpito wa mamlaka.

Muhtasari

•Ruto ameeleza kuwa aliwasiliana na rais huyo anayeondoka kwa njia ya simu na kujadiliana kuhusu masuala uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Rais wa tano wa Kenya
WILLIAM RUTO Rais wa tano wa Kenya
Image: Facebook//WILLIAMRUTO

Rais mteule William Ruto amefichua kuwa aliweza kuwasiliana na rais Uhuru Kenyatta kufuatia kuidhinishwa kwa kuchaguliwa kwake kama rais wa tano wa Kenya.

Ruto ameeleza kuwa aliwasiliana na rais huyo anayeondoka kwa njia ya simu na kujadiliana kuhusu masuala uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wawili hao pia waliweza kujadili mchakato wa mpito wa mamlaka.

"Nilishiriki mazungumzo ya simu na bosi wangu, Rais Uhuru Kenyatta. Tulijadili Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi punde na mpito kama inavyotarajiwa na mila na desturi zetu za kidemokrasia," Ruto alisema kwenye Twitter.

Siku ya Jumatatu rais mteule alidai kwamba hajaweza kuwasiliana na Uhuru katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita.

Ruto hata hivyo alidokeza kuwa angepiga hatua ya kumpigia simu rais huyo anayeondoka ili kujadili mpito.

"Nitampigia simu Rais Uhuru Kenyatta, Hatujazungumza kwa miezi kadhaa lakini hivi karibuni nitapiga simu ili tufanye mazungumzo kuhusu mchakato wa mpito," alisema.

Rais mteule alikuwa akizungumza nyumbani kwake Karen, Nairobi baada ya mahakama ya upeo kuidhinisha ushindi wake.

Hayo yalijiri licha ya kwamba Ruto alitangazwa kuwa Rais mteule na tume ya uchaguzi na mipaka mnamo Agosti 15.

Kjadi, inatarajiwa kuwa rais aliyeko madarakani angemshirikisha rais mteule katika masuala ya mpito.