Sijawahi kuyaona! Moses Kuria akana makubaliano ya Ruto, Mudavadi na Wetangula

Muhtasari

•Kuria alikiri hajawahi kuona makubaliano yanayopendekeza kuwa  eneo la Magharibi litapata asilimia 30 ya serikali ya Kenya Kwanza ikiwa viongozi hao wawili kutoka upande huo watawasilisha 70% ya kura.

•Kuria ameeleza kuwa chama chake cha CCK kilikubali kushirikiana na vyama vingine vya Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi wa Agosti.

Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Image: MAKTABA

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ameweka wazi kuwa hafahamu undani wa mkataba wa makubaliano kati ya Ruto na kinara wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Masika Wetangula.

Akizungumza katika runinga ya Citizen Jumapili jioni, Kuria alikiri hajawahi kuona makubaliano yanayopendekeza kuwa  eneo la Magharibi litapata asilimia 30 ya serikali ya Kenya Kwanza ikiwa viongozi hao wawili kutoka upande huo watawasilisha 70% ya kura.

Mgombea ugavana huo wa Kiambu kwa tikiti ya Chama Cha Kazi (CCK) alidai kuwa amekuwa akisikia tu kuhusu makubaliano hayo kama Wakenya wengine.

"Sijaona makubaliano hayo, sijawahi kuona makubaliano hayo ya 30%. Huwa nasikia tu kuyahusu. Sijawahi kuona makubaliano ambayo ANC ilitia saini," Kuria alisema.

Ruto, Mudavadi na Wetangula tayari wamekiri kuwa makubaliano hayo yapo na wamekuwa wakiyazungumzia wakati wakifanya kampenzi zao katika mikutano mbalimbali ya kisiasa.

Kuria ambaye amejitokeza kulalamika dhidi ya chama cha Ruto cha UDA akidai kinadhulumu vyama vingine ameeleza kuwa chama chake cha CCK kilikubali kushirikiana na vyama vingine vya Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi wa Agosti.

"Tutashiriki katika kuunda serikali. Itakuwa serikali yetu. Hiyo ndio maana tunatafuta kura kama vyama vingine kama UDA, Ford Kenya na ANC," Alisema.

Mbunge huyo hata hivyo hakubainisha asilimia ya serikali ambayo chama chake kingepata ikiwa muungano wa Kenya Kwanza utatwaa ushindi.

Alifichua kuwa juhudi ya vyama ndiyo itatathmini asilimia ya serikali ambayo vitanufaika nayo katika serikali ya Ruto.

"Ndio maana tunalalamika kuhusu juhudi zetu kudhoofishwa.Kwa kudhoofisha juhudi zetu unaenda kinyume na maslahi yetu kwa muungano," Kuria aliteta.

Kiongozi huyo ameibua madai kuwa chama cha UDA kimekuwa kikidhalilisha vyama shirika katika muungano wa Kenya Kwanza.

Wiki iliyopita Kuria kwa kushirikiana na mshindani wake katika kinyang'anyiro cha ugavana wa Kiambu William Kabogo waliandika barua wakilalamika kuhusu jinsi juhudi za vyama vyao zimekuwa zikidhoofishwa.