Uhuru Kenyatta ana haki ya kumuidhinisha mrithi wake- Jakaya Kikwete

Kikwete alisema Uhuru ana haki ya kufanya maamuzi ya kumpigia kura nan

Muhtasari

•Jakaya Kikwete amemtetea Rais Uhuru Kenyatta kuhusu uamuzi wake wa kuunga mkono Azimio la Umoja.

•Kikwete ataongoza timu ya waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 nchini Kenya.

katika picha ya maktaba
Aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete katika picha ya maktaba
Image: MAKTABA

Rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete amemtetea Rais Uhuru Kenyatta kuhusu uamuzi wake wa kuunga mkono Azimio la Umoja.

Kikwete alisema Uhuru ana haki ya kufanya maamuzi ya kumpigia kura nani.

“Rais Uhuru kujihusisha katika uchaguzi ni sawa, yeye pia ni Mkenya, ana haki ya kutoa mawazo yake,” alisema.

Rais huyo mstaafu alizungumza jijini Nairobi siku ya Jumatatu.

Matamshi yake yalikuja huku kukiwa na ongezeko la wito kutoka kwa Naibu Rais William Ruto kumtaka Uhuru kutojihusisha na siasa za mpito na kumwacha ashughulike na mgombea urais wa Azimio Raila Odinga.

Uhuru alimuidhinisha Raila kama mrithi wake anayependelea zaidi, hatua ambayo ilionekana kama usaliti na Ruto ambaye alikuwa mwandani wake wa kisiasa aliyegeuka mkosoaji.

Lakini Kikwete alisema rais anayemaliza muda wake ana haki kwa nafasi yake kama raia wa Kenya kushirikiana kisiasa na yeyote ampendaye.

"Rais Uhuru kujihusisha na uchaguzi ni sawa, ni mkenya na ana haki ila mimi sioni tatizo lolote yeye kuamua kuungana na mtu."

Rais huyo wa zamani wa Tanzania ambaye aliwasili nchini Jumatatu ataongoza timu ya waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 nchini Kenya.

Timu hiyo ilijumuisha waangalizi wapatao 52 kutoka nchi wanachama wa EAC ambao watakuwa nchini kuanzia Agosti 1 hadi Agosti 12, 2022, kuangalia uchaguzi huo.

Kikwete alibainisha kuwa Kenya imedumisha amani katika kipindi cha kampeni.

"Pongezi nyingi kwa Wakenya kwa kuwa watulivu hadi kufikia hatua hii ambapo kampeni ziko kwenye kilele," Kikwete alisema.

Aliwataka Wakenya kudumisha amani hata baada ya uchaguzi.

Utafsiri: Samuel Maina