Wafuasi wa Ngirici wafurushwa kutoka kituo cha kuhesabia kura kutumia vitoa machozi

Wafuasi hao walijaribu kuingia kwa nguvu katika kituo cha kuhesabia kura cha shule ya upili ya Kianyaga.

Muhtasari

•Maafisa wa polisi walilazimika kufyatua gesi ya kutoa machozi kwa kundi la wafuasi wanaoegemea upande wa mgombeaji wa ugavana wa Kirinyaga Wangui Ngirici.

•Wafuasi wa Ngirici walijaribu kuvamia kituo hicho huku wakirusha mawe baada ya kuhisi kuna kitu kisicho cha kawaida kuhusu ujumuishaji wa kura.

Kitoa machozi
Kitoa machozi
Image: MAKTABA

Polisi waliwarushia vitoa machozi wafuasi wa Ngirici kwa kujaribu kuvamia kituo cha kuhesabia kura katika eneo bunge la Gichugu.

Afisa wa polisi walilazimika kufyatua gesi ya kutoa machozi kwa kundi la wafuasi wanaoegemea upande wa mgombeaji wa ugavana wa Kirinyaga Wangui Ngirici.

Hii ni baada ya wafuasi hao kujaribu kuingia kwa nguvu katika shule ya upili ya Kianyaga ambayo ni kituo kikuu cha kuhesabia kura eneo bunge la Gichugu.

Kulingana na msimamizi wa uchaguzi katika eneo bunge hilo Geoffrey Gitobu,Virugu ilianza pale mmoja wa maafisa wasimamizi alipojaribu kuruka foleni ndefu iliyotengenezwa na maafisa hao walipokuwa wakirudisha matokeo ya kura katika kituo cha kujumlisha kura.

Haya yalijiri wakati afisa wa IEBC alitumia lango lingine katika kituo hicho akiwa amebeba vifaa vyake vya uchaguzi ili ahudumiwe haraka.

Kutokuwa na subira kwake inasemekana hatimaye kumesababisha hasara kubwa kwani hatua hiyo ambayo haikutarajiwa ilisababisha mzozo kati ya maajenti wanaoegemea upande wa gavana wa kaunti Ann Waiguru na mgombeaji wa kujitegemea Wangui Ngirici ambao wamekuwa katika ushindani mkali.

Wafuasi wa Ngirici walijaribu kuvamia kituo hicho huku wakirusha mawe na kupelekea msongamano wa magari katika barabara ya Kutus-Kianyaga baada ya kuhisi kuwa kuna kitu kisicho cha kawaida kuhusu ujumuishaji wa kura.

Hata hivyo, juhudi zao zilitatizwa na maafisa wa usalama waliokuwa tayari wamejihami na wenye macho ya mwewe ambao walituliza hali hiyo.

Kamanda wa polisi wa  kaunti  hiyo Mathews Mang'ira alionya wanasiasa dhidi ya kuwachochea wafuasi wao kufanya vurugu.