Stori za Ghost: Mchuuzi auma mteja sikio kwa kutonunua ovacado baada ya kuzifinya

Ghost amesema kuwa jamaa huyo alishtakiwa na kufikishwa katika mahakama ya Kibera alikoachiliwa kwa dhamana ya Sh 100,000.

Muhtasari

•Kulingana na Ghost, mchuuzi huyo ambaye ni mwenye kukasirika upesi hakuridhishwa na kitendo hicho na baada ya kuchemkwa na ghadhabu akamuua sikio mteja huyo.

•Ghost ameshauri Wakenya kusita kugusagusa mali ya wauzaji ikiwa hawana nia ya kununua.

ghost
ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost kitengo cha Stori za Ghost alfajiri ya Jumanne, mtangazaji wetu Ghost Mulee amesimulia kuhusu tukio moja ambapo hasira za mchuuzi  mmoja zilimsukuma kuuma sikio la mteja wake.

Kama mwanamuziki Mejja alivyoiba  kwenye kibao chake 'Tabia za Wakenya', kunazo baadhi za tabia za kipekee za Wakenya. Moja ya hizo tabia ni kubofyabofya maparachichi kila wanapoenda kuyanunua sokoni ili kubaini ikiwa yameiva.

Basi tabia hiyo imemletea shida mkazi mmoja wa jiji la Nairobi ambaye alibofya maparachichi ya mchuuzi mmoja kisha  akakosa kununua.

Kulingana na Ghost, mchuuzi huyo ambaye ni mwenye kukasirika upesi hakuridhishwa na kitendo hicho na baada ya kuchemkwa na ghadhabu akamuua sikio mteja huyo.

"Juzi hapa mtaani jamaa ameenda anataka kununua ovacado. Ameenda akaangalia, unajua wale wachuuzi huwa wametulia pale mteja anapofanya shughuli yake. Jamaa amekuja akashikashika ovacado, mara akasema eti sinunui. 

Muuza ovacado ambaye alikuwa mwepesi wa hasira akamuuliz, 'Na unashikashika ovacado zangu kwa nini kama hununui? Si ungeziangalia kwa macho. Mbona unazibonyezabonyeza? Sasa unafikiri nani atanunua hizi ovacado ambazo wewe umeshikashika karibu dakika tano'?

Hapo huyo mchuuzi akamuuma sikio huyo jamaa" 

Ghost amesema kuwa jamaa huyo alishtakiwa na kufikishwa katika mahakama ya Kibera alikoachiliwa kwa  dhamana ya Sh 100,000.

"Alipelekwa  mahakama ya Kibera na kutoka na dhamana ya 100,000 " Ghost alisimulia.

Ghost ameshauri Wakenya kusita kugusagusa mali ya wauzaji ikiwa hawana nia ya kununua.

"Tafadhali Wakenya, hii tabia ya kugusagusa mali ya watu na hununui wachana nayo. Afadhali uulize bei ni ngapi kwa mbali haswa chakula kwa kuwa zinaharibika haraka" Ghost alisema.