Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Constance Gakii (25) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Gideon Mulii (32) ambaye walikosana wiki iliyopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.
Gakii alieleza kwamba mzozo uliibuka wakati aliamua kuuza kuku wa familia bila idhini ya mumewe.
"Ilikuwa wiki iliyopita wakati mzee wangu alinituma nikauze kuku wawili ili tuweze kununua kuku wengine. Baada ya kuwauza akaniambia nimsaidie kulipa mkopo na pesa zile. Kulikuwa na shida kubwa pale nyumbani kwa hivyo nikaamua kuuza jogoo mmoja" Gakii alisimulia.
Gakii hakufahamisha mumewe mara moja kwamba alikuwa ameuza jogoo mmoja kati ya wawili waliokuwa pale nyumbani na Mulii alikuja kugundua baadae wakati alipopiga simu nyumbani asubuhi moja na kusikia sauti ya jogoo mmoja tu akiwika.
Mwanadada huyo alieleza kwamba bwana yake alikasirika sana alipoarifiwa kuwa jogoo mmoja alikuwa ameuzwa ili kusuluhisha tatizo la pesa pale nyumbani.
"Jogoo walikuwa wawili na alikuwa akikataa niuze lakini nikasema niuze tu mmoja. Siku moja alipopiga simu asubuhi alisikia jogoo mmoja tu akiwika akaniuliza mwingine ako wapi nikamwambia niliuza. Nilipomueleza hayo aliniambia kuwa huwa nakataa kusikiza maneno yake. Nilimwambia kwamba niliuza kwani kulitokea tatizo la pesa" Gakii alisimulia.
Licha ya kuelezwa kilichokuwa kimetokea, Mulii hakuridhika na akaamua kumfukuza mkewe nyumbani.
"Aliniambia nichukue vitu zangu niende eti kwa sababu huwa simheshimu. Kutoka hapo huwa hashiki simu zetu. Yeye hufanya kazi nyumbani na sisi tuko nyumbani" Gakii alisimulia.
Juhudi za kuwapatanisha wanandoa hao hata hivyo ziligonga mwamba kwani Mulii alikosa kuchukua simu licha ya Gidi kujaribu kumpigia mara kadhaa.
Gakii alieleza kwamba mumewe ako na mazoea ya kukataa kushika simu zake kila wanapokosana.
Wawili hao wamekuwa kwa ndoa kwa miaka sita na tayari wamebarikiwa na watoto wawili.