Stori za Ghost: Mjane auza shamba la familia mwanawe akiwa tayari amejenga ili akaponde raha kwingine

Muhtasari

•Inasemekana kwamba mume wa mwanamke huyo alipokuwa hai alikuwa amemzoesha maisha ya raha  kwani mara kwa mara wawili hao wangeenda kujiburudisha katika maeneo mbalimbali ya burudani.

•Kizaazaa kikubwa kilitimbuka pale huku mwanamke yule akimwarifu mwanawe kwamba yeye ndiye aliyeachiwa shamba na mumewe kwa hivyo alikuwa na madaraka ya kuliuza.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Stori za Ghost, mtangazaji Ghost Mulee alisimulia kisa kimoja ambacho kilijitokeza katika eneo la Luanda kaunti ya Vihiga.

Ghost alisimulia jinsi mjane mmoja aliacha mwanawe katika hali ya mshangao baada ya kuuza shamba ya familia ambapo amekuwa akiishi.

Inasemekana kwamba mume wa mwanamke huyo alipokuwa hai alikuwa amemzoesha maisha ya raha  kwani mara kwa mara wawili hao wangeenda kujiburudisha katika maeneo mbalimbali ya burudani.

Kwa kuwa mjane huyo alikuwa amepeza maisha hayo akaamua kuuza shamba ya familia ili aweze kugharamia burudani aliyotaka.

"Kijana alikuwa amejenga nyumba kwa ile shamba wakati babake alipokufa. Lakini mama alimuuliza mbona hajawahi kumfanyia chochote kwa wakati wote ambapo aliishi pale ilhali babake alipokuwa  hai alikuwa anampeleka kuponda raha kila wikendi. Akwambia kwamba alikuwa ameuza shamba ile" Ghost alisimulia.

Kwa wakati huo huo walipokuwa wanapiga gumzo, kijana yule aliona watu wageni wakija kuchukua umiliki wa shamba lile huku wakidai kwamba tayari walikuwa wamelilipia.

Kizaazaa kikubwa kilitimbuka pale huku mwanamke yule akimwarifu mwanawe kwamba yeye ndiye aliyeachiwa shamba na mumewe kwa hivyo alikuwa na madaraka ya kuliuza.

"Mjane huyo alieleza kwamba aliamua kuuza shamba hilo ili aweze kuhamia mahali kwingine ambako angeendelea kuponda raha" Alisimulia Ghost.

Kijana yule aliachwa pale asijue la kufanya kwani kwa kweli jina la mama yake ndilo lililokuwa limenakiliwa kwenye hati ya hatimiliki ya shamba hilo.