Mwanadada aliyedanganya kifo ili aachane na mpenziwe baada yake kufilisika ataka kumrudia

Muhtasari

•Alitumia nambari mpya ya simu akaandikia mpenzi wake ujumbe kuhusu 'kifo na mazishi' yake huku akijifanya binamu yake.

•Jamaa aliendelea kuomboleza 'kifo' cha mpenzi wake kwa muda huku akipakia kumbukumbu za mapenzi yao.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi siku ya Alhamisi, shabiki mmoja alituma ujumbe akiomba kupata ushauri.

Mwanadada huyo ambaye hakutaka kutajwa jina alisema alikuwa kwenye mahusiano na jamaa mmoja ambaye hakuwa sawa kimfuko ila walipendana sana.

Baada ya kuvumiliana kwa miezi kadhaa jamaa alifanikiwa kupata kazi na akawa na uwezo wa kukimu mahitaji ya pale nyumbani.

Hata hivyo mwaka uliopita wakati janga la Corona liliingia nchini jamaa alianza kufilisika tena na hilo likamshinikiza mwanadada yule kutaka kutema mpenziwe.

Baada ya kuwaza sana kuhusu njia ambayo angetumia kumuacha mpenzi wake mwanadada huyo aliamua kudanganya kifo chake.

Alitumia nambari mpya ya simu akaandikia mpenzi wake ujumbe kuhusu 'kifo na mazishi' yake huku akijifanya binamu yake.

Katika ujumbe huo, alieleza mumewe kuwa kwa sababu ya mikakati iliyokuwa imewekwa kudhibiti maambukizi ya Corona 'mazishi' yake yangehudhuriwa na wanafamilia wachache tu na tayari orodha ilikuwa imetengenezwa bila yeye kuwepo.

Baada ya 'mazishi' kufanyika mwanadada huyo aliendelea kufuatilia jamaa huyo kwenye mtandao wa Facebook.

Jamaa aliendelea kuomboleza 'kifo' cha mpenzi wake kwa muda huku akipakia kumbukumbu za mapenzi yao.

Siku ziliposonga jamaa alianza kufanikiwa tena kifedha na  kuanza kupakia picha zilizoonyesha ziara mbalimbali alizofanya.

Kufuatia hayo mwanadada huyo akatamani kumrudia mpenzi wake ila tatizo ni kuwa tayari alikuwa 'amekufa'.

Je, una ushauri upi kwa mwanadada huyu?