Shabiki amletea Gidi mafuta studioni baada ya gari lake kukwama akija kazini

Muhtasari

•Jessy aliwasili studioni mwendo wa saa moja asubuhi ya Alhamisi akiwa amebeba bidhaa hiyo adimu kote nchini kwenye mtungi wa lita 20.

•Gidi alikumbana na changamoto alipokuwa akiendesha kuja kazini baada ya gari lake kuisha mafuta.

Jessy amletea Gidi mafuta katika studio za Radio Jambo
Jessy amletea Gidi mafuta katika studio za Radio Jambo

Shabiki mmoja wa Radio Jambo alimuacha mtangazaji  wa kipindi cha  Gidi na Ghost Asubuhi, Gidi Ogidi na tabasamu kubwa baada ya kumletea mafuta ya gari katika studio zetu.

Jessy aliwasili studioni mwendo wa saa moja asubuhi ya Alhamisi akiwa amebeba bidhaa hiyo adimu kote nchini kwenye mtungi wa lita 20.

Huku akiwa amejawa na bashasha isiyoelezeka, Gidi alimshukuru shabiki huyo na kumtakia baraka za Maulana.

"Jessy ni shabiki wa kipindi cha Gidi Na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo. Alisikia kuhusu shida zangu na ameniletea lita 20 za mafuta kwa studio. Ahsante sana Jessy. Wewe ni shabiki wa kweli na Mungu akubariki," Gidi alisema.

Alhamisi asubuhi, Gidi alikumbana na changamoto alipokuwa akija kazini baada ya gari lake kuisha mafuta.

Alitangaza masaibu yake kupitia mitandao ya kijamii na Meneja Mkuu wa Radio Africa, Martin Khafafa akajitolea kumsaidia kufika kazini.

Mkurugenzi mkuu wa Radio Africa Martin Khafafa akiwa na Gidi baada ya kuwasili kumsaidia wakati gari lake lilikwama kutokana na ukosefu wa mafuta.
Mkurugenzi mkuu wa Radio Africa Martin Khafafa akiwa na Gidi baada ya kuwasili kumsaidia wakati gari lake lilikwama kutokana na ukosefu wa mafuta.
Image: GIDIFACEBOOK

Wakenya kwa muda sasa wamekuwa wakihangaika kutokana na uhaba mkubwa wa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta taa kote nchini.

Juhudi za serikali kukwamua wakenya kutoakan na tatizo hilo zimeonekana kutozaa matunda huku foleni ndefu zikishuhudiwa kote nchini katika vituo vichache ambavyo vina mafuta. 

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO.