Gidi atumia ziara yake ya Uingereza kushuhudia soka moja kwa moja

Muhtasari

•Gidi alisafiri siku ya Ijumaa na ameonekana akinasa kila hatua ya ziara hiyo na kutoa taarifa kwa mashabiki wake.

•Gidi alishuhudia Liverpool ikinyakua kikombe cha FA kupitia matuta ya penalti baada ya mechi hiyo kuishia sare ya 0-0.

Mtangazaji Gidi nje ya uwanja wa Emirates siku ya Ijumaa
Mtangazaji Gidi nje ya uwanja wa Emirates siku ya Ijumaa
Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi Gidi Ogidi yuko kwenye ziara ya likizo nchini Uingereza.

Gidi alisafiri siku ya Ijumaa na ameonekana akinasa kila hatua ya ziara hiyo na kutoa taarifa kwa mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii.

Kilichoonekana kumvutia Gidi zaidi nchini Uingereza ni soka. 

Mtangazaji huyo alihudhuria mchuano mkali wa fainali ya kombe la FA kati ya Liverpool na Chelsea ambao ulichezwa  ugani Wembley Jumamosi 

Gidi alishuhudia Liverpool ikinyakua kikombe hicho kupitia matuta ya penalti baada ya mechi hiyo kuishia sare ya 0-0.

Baadae Gidi alipongeza vijana hao wa Jurgen Kloop kupitia ukurasa wake wa Instagram.

"Hongera Liverpool na hasa Sadio Mane licha ya kukosa penalti," Gidi aliandika chini ya picha za tiketi za kuhudhuria mechi hiyo.

Gidi pia alifanya ziara katika Uwanja wa Emirates wa klabu ya Arsenal na kupakia video na picha kadhaa alizochukua.

Katika video moja mtangazaji huyo aliwarekodi wazungu wakikimbia kupanda na kushuka ngazi zilizoko nje ya uwanja huo wa Emirates. Gidi aliwaagiza Wakenya kuiga mfano wa wazungu hao na kuwa wanafanya mazoezi mara kwa mara.

"Lo, watu hawa kwa kawaida huja kukimbia hapa kila siku. Kwenye ngazi za Emirates.Njia nzuri ya kufanya mazoezi." Gidi alisema.

Gidi yuko kwenye likizo fupi na anatarajiwa kurejea hewani hivi karibuni.