Mwanasoshalaiti Vera Sidika alikuwa mgeni wetu katika kipindi cha Bustani la Massawe, kitengo cha Ilikuaje? mnamo siku ya Ijumaa.
Katika kipindi hicho, Vera alifunguka kuhusu masuala mengi yakiwemo mahusiano yake na hatua mpya ya uzazi.
Mke huyo wa Brown Mauzo aliweka wazi kuwa kwa sasa kazi yake kubwa ni kulea binti yake wa mwaka mmoja.
"Kwa sasa nimeangazia mtoto wangu na kuangalia afya yake," alisema.
Alibainisha kuwa anaweza kumnyonyesha vizuri binti yake Asia Brown bila matatizo yoyote licha ya kuwa na vipandikizi vya matiti.
Alisema kuwa aliamua kufanyiwa upasuaji wa kuongeza ukubwa wa matiti yake kwa sababu alihisi mwili wake haukuwa sawia.
"Mimi ni mzaliwa wa Pwani. Nimezaliwa nikiwa nimejaliwa na makalio makubwa lakini sikujaliwa na matiti. Nilihisi siko sawia," alisema.
Aliongeza ,"Nilikaa nikasema kwa sababu sasa najiweza naweza kuenda nje ya nchi na kufanyiwa upasuaji,"
Mwanasoshalaiti huyo alibainisha kuwa mchakato wa kupandikiza matiti ambao alifanyiwa si wa kudumu na unaweza kutenduliwa.
Pia alibainisha kuwa alichagua mchakato ambao hungeathiri uzazi wake kwa kuwa alitazamia kuwa na mtoto katika siku za usoni.
"Naweza kunyonyesha kawaida," alisema.