Mtangazaji Gidi amuomboleza mwanafamilia wake mdogo

Pendo ,7, alikata roho mwendo wa saa mbili usiku, siku ya Jumapili.

Muhtasari

•Gidi alifichua kwamba mpwa wake Pendo aliaga dunia siku ya Jumapili jioni katika Hospitali ya Metropolitan.

•Gidi aliongeza kuwa familia itatoa maelezo zaidi kuhusu mipango na tarehe ya mazishi hivi karibuni

Mtangazaji Gidi Ogidi

Mtangazaji mkuu wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi amefiwa na mpwa wake.

Gidi alifichua kwamba Baby Pendo ambaye ni binti pekee wa dada yake aliaga dunia siku ya Jumapili jioni katika Hospitali ya Metropolitan.

Pendo ambaye alikuwa na umri wa miaka 7 tu alikata roho mwendo wa saa mbili usiku, siku ya Jumapili.

"Tulikuwa na usiku mrefu lakini wacha nishukuru hospitali, jirani yangu Wakili na marafiki ambao walituunga mkono katika mchakato wa kuhamisha mwili wake hadi chumba cha kuhifadhi maiti," Gidi alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatatu asubuhi.

Mtangazaji huyo mahiri aliongeza kuwa familia itatoa maelezo zaidi kuhusu mipango na tarehe ya mazishi hivi karibuni.

Pia alifahamisha mtu yeyote aliye na nia ya kutoa msaada wa aina yoyote kwa maziko ya mpwa wake kuwasiliane naye.

"Roho ya Mtoto Pendo ipumzike kwa amani,” alisema.

 Sote katika Radio Jambo tunaitakia familia ya Gidi amani na nguvu na wanapomuomboleza mmoja wao. Roho ya Pendo ipumzike kwa amani.