Mtangazaji wa Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi amejawa na bashasha baada ya kugundua kuwa tumbo lake limepungua.
Siku ya Jumatatu asubuhi, Gidi ambaye ni mtangazaji mkuu wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi alionyesha mwonekano wake wa sasa kwenye picha na kusema kuwa tumbo lake limepungua ukubwa.
Alidokeza kuwa amekuwa na tumbo lililochomoza kwa muda mrefu huku akieleza kuwa lishe bora imemsaidia kupunguza.
"Tumbo langu linapotea, kumbe hili jambo la lishe linafanya kazi," alisema.
Mwimbaji huyo wa zamani alitumia fursa hiyo kuwashauri watu wengine kuzingatia lishe bora ili kuweka miili yao sawa.
"Angalia unachokula, kula kiafya, kuwa na afya njema 🙌," alisema.
Wiki iliyopita, mtangazaji huyo mahiri alikiri kwamba amepunguza uzito kiasi wa mwili katika siku za hivi majuzi.
Katika taarifa yake ya mtandao wa Instagram, Gidi alifichua kwamba alikuwa anaugua kwa muda siku kadhaa zilizopita.
Mtangazaji huyo wa kipindi cha asubuhi hata hivyo alibainisha kuwa kwa bahati nzuri, kwa sasa amepata nafuu kikamilifu.
"Habari za asubuhi, ndio nimepoteza kilo kadhaa, nilikuwa mgonjwa lakini sasa nimepata nafuu," alisema kupitia Instagram.
Kufuatia hilo, Gidi alitoa shukrani za dhati kwa Maulana kwa kumwezesha kurejesha afya nzuri baada ya kuugua.
Alidokeza kuwa aliugua baada ya kula chakula kilichoharibika na hivyo kuwaonya watu kuwa waangalifu na kile wanachokula.
"Jihadharini na muangalie kile mnachokula, kuharibika kwa chakula ni kweli," alisema.
Takriban wiki nne zilizopita, Gidi alifichua kwamba alikuwa amelazwa hospitalini baada ya kuugua.
Kwenye ukurasa wake wa Instagram, mtangazaji huyo alichapisha picha yake akiwa katika chumba cha wagonjwa huku akiwa na sindano kwenye mkono wa kushoto na akabainisha kuwa anapata nafuu.
"Siku ya tatu ya sindano ya IV, nahisi vizuri zaidi," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.
Kwa siku mbili, mashabiki wa kipindi maarufu cha Gidi na Ghost Asubuhi Radio Jambo asubuhi walikosa sauti ya Gidi huku mtangazaji mwenzake Ghost Mulee akiendesha kipindi hicho peke yake.