Mambo imechemka! Gidi ajawa wasiwasi kuhusu Arsenal kupoteza kombe la EPL

"Nimeangalia mechi zilizosalia mbele yetu. Sisi ni watu wanyenyekevu. Acha tu tubaki wanyenyekevu," alisema.

Muhtasari

•Siku ya Alhamisi asubuhi, Gidi alidokeza kwamba amekumbwa na hofu baada ya kutazama ratiba ya  michuano ijayo.

•Wanabunduki wanaongoza  jedwali kwa pointi 74 huku Man City wakishikilia nafasi ya pili kwa pointi 70.

Image: GIDI OGIDI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu mechi zilizosalia za klabu yake pendwa, Arsenal kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.

Siku ya Alhamisi asubuhi, Gidi alidokeza kwamba amekumbwa na hofu baada ya kutazama ratiba ya  michuano ijayo.

"Wueh, nimeangalia mechi zilizosalia mbele yetu. Sisi ni watu wanyenyekevu. Acha tu tubaki wanyenyekevu," alisema.

Mtangazaji huyo mahiri hata hivyo alidokeza kuwa bado ana imani na klabu yake huku akieleza kuwa Mola bado anatawala.

 "Mambo imechemka! Lakini tunabaki wanyenyekevu, Mungu mbele," alisema.

Kauli ya Gidi inajiri masaa machache tu baada ya washindani wakuu wa Wanabunduki katika EPL, Manchester City kufuzu kwa nusu fainali ya kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya. 

Vijana wa Pep Guardiola waliingia kwenye hatua ya nusu fainali siku ya Jumatano usiku baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mechi ya robo fainali ya mkondo wa pili na Bayern Munich ya Ujerumani ugani Allianz Arena. Katika mechi ya mkondo wa kwanza wiki iliyopita, Man City iliwaadhibu Bayern 3-0.

Kwenye EPL, Wanabunduki bado wanaongoza  jedwali kwa pointi 74 baada ya kucheza mechi 31 huku Man City wakishikilia nafasi ya pili kwa pointi 70 ambazo wamezoa kutoka mechi 30 ambazo wameshiriki.

Vilabu hivyo viwili vinatarajiwa kumenyana kwenye Uwanja wa Etihad wiki ijayo, Aprili 26, katika mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa na ambayo inatazamiwa kucheza nafasi kubwa katika uamuzi wa mshindi wa kombe la EPL 2022/23.