Peter Onkari ,25, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Shiro Wanjiku ,21, ambaye alitengana naye takriban miaka miwili iliyopita.
Onkari alisema Shiro aliondoka kwenda kusalimiana na watu wa familia yake mwaka wa 2021 lakini hajawahi kurudi tangu wakati huo
"Shiro alikuwa bibi yangu tulikaa miaka miwili. Tulipata mtoto mmoja. Alifunga safari ya kuenda kwao. Tangu aende hajawahi kurudi, miaka miwili imepita. Nikimuuliza anasema harudi Kisii. Nataka nijue kama ameniacha," Onkari alisimulia.
Aliendelea, "Tulipatana naye mjini Nakuru na akakubali tukae naye. Hapo awali tulikuwa tunaishi Narok. Kumpeleka nyumbani kwetu Kisii akasema aende nyumbani asalimiane kwanza, hajawahi kurudi."
Onkari alidokeza kuwa baba mkwewe alikuwa anapinga sana bintiye aolewe naye. Pia alidokeza kuwa hajakuwa akishughulikia majukumu ya mkewe na mtoto wao tangu mzazi huyo mwenzake alipotoroka.
"Huko kwao, baba yake alikuwa anakata asioleke. Alikuwa anakataa kabisa. Yeye hakuwa na shida ya kuenda Kisii. Babake ndo alikuwa anamwambia asiloewe huko. Wakati alienda kwao sijawahi kumshughulikia," alisema.
Shiro alipopigiwa simu aliweka wazi kuwa tayari alimtema mzazi huyo mwenzake na kubainisha kuwa hisia za mapenzi ziliisha.
"Nilimuacha, juu sitaki kuendelea na yeye tena. Hakuwa ananipiga. Hata wazazi wangu walipinga hiyo kitu. Nilikuwa nampenda lakini saa hii mapenzi yaliisha," Shiro alisema.
Aliendelea, "Saa hii mtoto ako na miaka tatu lakini hajawahi kutaka kujua anaendelea aje. Nilitoka mtoto akiwa na mwezi moja. Hisia ziliisha. Tulikuwa tunapendana lakini dadake alikuwa anaingilia ndoa. Alikuwa anafanya kazi huku alikuwa ashajulikana tabia zake. Hata alikuwa ashawahi kuleta bibi mwingine huyo. Akipigiwa simu akuje nyumbani anasema tu anakuja. Imepita miaka minne sasa anasema tu anakuje."
Mwanadada huyo alimbainishia mzazi huyo mwenzake kwamba hawezi kurudi katika ndoa yao kama Onkari hajapiga hatua ya kuenda nyumbani kwao ili kuzungumza na wazazi wake.
"Wewe enda muelewana na wazazi kwanza. Lakini hata siwezi kurudi juu mapenzi yangu yaliisha kitambo," alisema.
Onkari alieleza hofu yake kuwa wakwe zake hawakutaka kumuoana nyumbani kwao.
Hata hivyo, alibainisha kuwa sasa atasonga mbele na maisha yake kwa kuwa tayari amejua msimamo wa Shiro.
"Nishajua msimamo wake. Nitajua cha kufanya. Hasemangi iko aje mtu ajue cha kusema. Huyo hakaangi nyumbani. Kuna ndugu yake huwa tunazungumza naye. Mtoto ako Nyandarua lakini yeye ako Kirinyaga. Mtoto sijawahi kushughulikia," alisema.
Ushauri wako kwa wawili hao ni upi?