Mwanadada ambaye alijitambulisha kama Jesca Adhiambo ,22, kutoka kaunti ya Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Meshack Makoha ,28, ambaye alitofautiana naye siku ya Jumanne.
Jesca alisema wasiwasi uliingia katika ndoa yao ya miaka minne wakati mumewe alipomkasika baada ya yeye kuenda ushirika bila idhini yake.
"Ilikuwa jana, saa tisa nilimwambia nataka kutoka naenda ushirika. Akauliza nimeingia kanisa hivi majuzi na nimeanza ushirika vipi. Akaniambia hakuna mahali nitaenda. Nikamuomba niende kwa sababu nilikuwa nishaambia wenzangu naenda. Mimi nilitoka tu nikaenda. Nilitoka huko kitu saa kumi na mbili jioni. Kufika kwa nyumba alikuwa tu amekasirika. Hajazungumza na mimi tangu wakati huo," Jesca alisimulia.
Aliongeza, "Tulikuja reserve ikabidi nikuje niangalie kanisa ambaye naweza kuenda, si kanisa ambayo nilikuwa naenda nikiwa town. Nilienda ushirika na mtoto mdogo nikamuachia mkubwa. Nilienda baada ya kutayarisha lunch na breakfast. Najua hiyo ndo kitu ilifanya nikasirika."
Jesca alifichua kuwa leo asubuhi, Jumatano, mumewe alitoka akaenda kazini bila kunena naye chochote.
"Ameenda kazini bila kuniongelesha. Chakula amekula tu. Hata chai amekunywa tu na haongei. Ukimkosea kidogo tu huwa anakasirika," alisema.
Meshack alipopigiwa simu alitupilia mbali madai ya kukasirika na kudai kwamba yuko sawa.
"Sio eti nilikuwa nimenuna. Kuna jamaa tulikuwa tumefanyia kazi na hakuwa ametulipa. Kurudi nyumbani nilijaribu kumuongelesha," Meshack alisema.
Aidha, alibainisha kuwa wazazi wake hawako sawa na mkewe kuhudhuria kanisa ambayo amechagua kuwa anaenda.
"Wazazi hawataki aende hiyo kanisa. Wanasema sisi tuko Illuminati. Mimi nilimwambia awe tu anaenda. Huwa anaenda ushirika na huwa simkazii. Hata hivyo wazazi wameleta shida sana. Mimi nikamwambia angoje kidogo. Yeye hajapendezwa na kanisa ya wazazi wangu. Mimi ndio nilimwambia aende hiyo kanisa. Mimi sina shida na hiyo kanisa. Nilikwambia nimekasirika mambo na kanisa sio mambo na kanisa," alisema.
Jesca hata hivyo alimlalamikia, "Kuwa kawaida asubuhi huwa unanigusa unaambia ukienda kazini. Lakini leo nimeshtukia tu mlango imefungwa nikashindwa kwani nimelala tu peke yangu."
Kuhusu sababu yake kutoenda kanisa moja na wazazi wakwewe, Jesca alisema, "Tulikuwa tunaenda kanisa moja na wazazi wake lakini haikunipendeza. Nikaamua kujiunga na nyingine."
Wawili hao waliweza kuelewana na Meshack akaahidi kuzungumza na mkewe wakati atakaporudi nyumbani kutoka kazini.
Je, kuna funzo gani kutoka kwa Patanisho ya leo?