Katika ipindi cha Gidi na Ghost asubuhi ya Ijumaa kwenye kitengo cha Patanisho, mrembo kwa jina Belvyne Joy mwenye umri wa miaka 21 kutoka Migori alitaka kupatanishwa na aliyekuwa mume wake Elvis Chumba, 24, kutoka Nakuru.
Joy alieleza kwamba anataka kupatanishwa na baba mwanawe ambaye walikuwa wameishi pamoja kwa kipindi cha miaka 4, akisema kuwa wakati Chumba anamfukuza nyumbani, hakumpa sababu yoyote wala kumtajia makosa ya kupelekea uamuzi huo.
“Tulikosana mwaka 2022 baada yake yeye kuamka siku moja na kuniambia nakutafutia nauli urudi kwenu bila kuniambia chochote,” Joy aliambia watangazaji Gidi na Ghost.
Alisema kwamba baada ya kujifungua mtoto, alikaa mwezi mmoja na nusu kabla ya mumewe kumuambia kwamba alitaka kumsindikiza ili kumuaga ili aende kuishi na mama yake.
Mrembo huyo alisema kwamba yeye ako tayari kurudi kwa ndoa yake hata bila kutumiwa nauli, akisema kwamba ako na nauli yake na anachotaka ni ndio ya mume wake ili kurudi.
Joy hata hivyo amekabiliwa na ugumu kwani Chumba amekuwa akimkwepa katika mazungumzo yao kwa njia ya siku kwa visingizio kwamba kampuni anayofanyia kazi ilimtuma mbali, na wakati mwingine akisema kuwa hana nafasi.
Kwa upande wake Chumba alipopigiwa simu, alisema kwamba ni vile yuko kazini kidogo na hajapata nafasi ya kumkaribisha mkewe ili kurudi nyumbani.
Mwanamume huyo alimwambia mkewe kwamba ni sawa kurudi lakini akakataa kuongea na yeye kupitia redioni huku akiahidi kwamba watazungumza pembeni.
“Niko tayari Joy atarudi, tutaongea na yeye kwa sababu sasa hivi niko kazini nashughulika na kazi. Kwa sasa anaweza ingia kwa gari arudi nyumbani,” Chumba alisema.
“Hakuna mtu mwingine mimi napenda kama wewe Joy,” Chumba aliongeza.
Joy ambaye alikuwa tayari ameshasema yuko tayari na nauli aliahidi kufunga safari muda huo ili kurudi kwa ndoa yake.