Boaz Wafula Lechumo mwenye umri wa miaka 25 kutoka kaunti ya Bungoma aliomba kupatanishwa na mke wake Karen Bahati mwenye umri wa miaka 22 ambaye anasema aliondoka nyumbani bila kukosana.
Lechumo aliomba Gidi na Ghost katika kitengo cha patanisho kwamba mkewe alisubiri ameondoka nyumbani naye akaondoka.
Alisema kwamba mkewe ni mtu ambaye anamsikiliza sana mama yake na pengine ndio maana walikuwa wanakwaruzana kidogo kwenye uhusiano wao.
“Shida ni ya kwamba anasikiza Mama yake sana. Tumekaa kwa ndoa kwa mwaka moja na miezi minane na tuna Mtoto mmoja. Kwa hivi sasa ako kwao. Nisaidieni Mabingwa nitashukuru,” Lechumo alisema.
“Alijifungua mwaka jana Septemba, mamake alikuja hospitali akaenda na yeye hata wakanyoa mtoto. Kwa mila yetu Waluhya inafaa mtoto anyolewe kwa kina mume. Tumekuwa tukivutana sana,” Lechumo alisema huku akisisitiza kwamba hakumpiga wala hawakugombana wakati anaondoka.
“Nimejaribu kumfuatilia arudi ananiambia mama yake ndio anamzuilia kutorudi,” aliongeza.
Lechumo alisema kwamba ameenda kujitambulisha kwa kina mke lakini bado mahari hajapata kulipa lakini akakiri kwamba wanaendelea kujipanga.
Mkewe Karen Bahati alipopigiwa simu, alimwambia mumewe hewani kwamba atafute barua aende kwao kama kweli anamtaka na anampenda.
Karen alifichua kwamba Lechumo alimtumia mama mkwe ujumbe kwamba hataki mambo na binti yake na kushangaa mbona tena alimpeleka kwa patanisho.
“Chenye utafanya, wazazi wamesema wananipeleka shule sijui kama nitarudi, acha tu nikulelee mtoto,” Karen alimwambia.
“Huyu jamaa hataki kuleta barua anataka afuatiliwe, sasa nimerudi shule nisome na nilee mtoto,” Karen aliwaambia Gidi na Ghost.
Watangazaji walimshauri Lechumo kujichanga na kupeleka barua ya kumuomba rasmi kutoka kwa wazazi wake na pengine kuanza mipango ya kulipa mahari.