Mwanariadha mashuhuri wa Kenya, Faith Kipyegon ameelezea furaha na shukrani zake tele baada ya kuchaguliwa kama ‘Star Person of The Year 2023’ katika tuzo za kila mwaka za gazeti la Star.
Faith ambaye nyota yake imeng'aa kwelikweli katika mwaka wa 2023 ambao unakaribia kuisha aliwashinda wateule wengine kadhaa kuwa chaguo bora zaidi la tuzo hiyo ya kifahari.
Wakati akiongea na mtangazaji wa Radio Jambo Bramwell Mwololo katika kipindi cha Ijumaa cha Gidi na Ghost Asubuhi, mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 29 aliweka wazi kwamba hakutarajia angeshinda tuzo hiyo.
“Nimeshukuru sana, sikuwa natarajia kuwa ‘Star Person of the Year’. Nawashukuru sana, nashukuru kila mtu kwa kunichagua,” Faith alimwambia Bramwell kupitia simu.
Alibainisha kuwa kushinda tuzo hiyo ya kifahari kumempa motisha ya kuendelea kufanya vyema zaidi katika kile anachofanya, riadha.
Mshikilizi huyo wa rekodi tatu za dunia aliweka wazi kuwa mazoezi mengi na kujiamini kumemsaidia kufikia mafanikio yote aliyoyapata mwaka huu na miaka ya nyuma.
“Vile nilianza nikiwa mdogo, nikikimbia pia mpaka leo. Nadhani nimeshindana na wasichana na wanawake wengine huko nje. Huwezi kuamka leo na uwe nyota, ni mchakato. Lazima upige hatua,” alisema Kipyegon.
Katika mahojiano hayo ya simu,Faith pia alifichua kuwa kando na kukimbia, amekuwa akifanya kilimo cha mimea na wanyama katika shamba lake mjini Eldoret.
Katika chapisho la kila siku la Ijumaa, Gazeti la The Star lilimtambulisha Faith Kipyegon kama ‘The Star Person of The Year’ (Mtu Nyota Bora wa Mwaka) likibainisha kuwa ndiye aliyependekezwa zaidi na umma, na pia kuidhinishwa na wahariri.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 29 alipata kura nyingi zaidi, rekodi ya uteuzi ya 228 kutoka kwa umma kati ya teuzi 2,123 ambazo zilipokelewa.
Kwa wahariri wa gazeti la Star ambao walikuwa na neno la mwisho, hili lilikuwa chaguo rahisi. Kwa kauli moja waliidhinisha uteuzi wa Kipyegon kama Mtu Nyota Bora wa Mwaka 2023.
Kipyegon alikubaliwa katika alama kwenye masanduku yote kulingana na sifa zilizokuwa zimetangazwa na Star.
Tuzo hilo la kifahari huwatambua watu ambao, miongoni mwa wengine, wamesaidia, wametia moyo au kuleta heshima kwa Kenya au wamejitahidi kuifanya Kenya kuwa mahali pazuri pa kuishi na kufanya kazi.