Mtangazaji Ghost Mulee afichua mipango yake ya Siku ya Wapendanao

Mtangazaji huyo alifichua kuwa tukio kuu ambalo ataadhimisha siku ya Jumatano, Februari 14 ni Jumatano ya Majivu.

Muhtasari

•Mtangazaji Ghost Mulee aliweka wazi kuwa amefurahi sana kwani itakuwa siku ambayo watakuwa wakiadhimisha mwanzo wa mfungo.

•Februari 14 ni siku maalum kwa wapendanao kote ulimwenguni kwani imetengwa mahususi kusherehekea mapenzi na kuthaminiana.

ndani ya studio za Radio Jambo.
Mtangazaji Jacob Ghost Mulee ndani ya studio za Radio Jambo.

Mtangazaji mcheshi wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob ‘Ghost’ Mulee hivi majuzi alifichua mipango yake ya siku ya wapendanao kwa mwanahabari Samuel Maina.

Huku akijibu maswali wakati wa mahojiano ya haraka, kocha huyo wa zamani wa Harambee Star alifichua kuwa tukio kuu ambalo ataadhimisha siku ya Jumatano, Februari 14 ni Jumatano ya Majivu.

Alibainisha kuwa yeye ni Mkatoliki na kuweka wazi kuwa amefurahi sana kwani itakuwa siku ambayo watakuwa wakiadhimisha mwanzo wa mfungo.

 “Hii Valentines ata nimefurahia sana kushukuru Baba Mtakatifu, kwa sababu hiyo ni siku yetu ya kuanza kufunga. Tunaanza kufungua siku hiyo, ni ash Wednesday,” Ghost Mulee alisema.

Tarehe 14 Februari kwa kawaida huwa ni siku maalum kwa wapendanao kote ulimwenguni kwani ni siku iliyotengwa mahususi kusherehekea mapenzi na kuthaminiana.

Siku ya Wapendanao pia inaitwa Saint Valentine's Day ama Feast of Saint Valentine.

Imepewa jina la mtakatifu wa Kikristo aliyefahamika kwa jina, Valentine.

Alikuwa askofu aliyefunganisha ndoa kati ya wanandoa waliokatazwa.

Walakini, kuna hadithi kadhaa za kifo cha kiimani kuhusiana na Saint Valentines zinazohusishwa na  Februari 14.

Baadhi ya hadithi pia ni pamoja na maelezo ya kufungwa kwa Mtakatifu Valentine wa Roma kwa ajili ya kuwahudumia Wakristo walioteswa chini ya Milki ya Kirumi katika karne ya tatu.

Kulingana na History Classics, hadithi nyingine zinaonyesha kwamba Valentine huenda aliuawa kwa kujaribu kuwasaidia Wakristo kutoroka magereza makali ya Waroma, ambako mara nyingi walipigwa na kuteswa.

"Kulingana na hadithi moja, Valentine aliyefungwa jela alituma salamu ya kwanza ya 'valentine' baada ya kumpenda msichana mdogo labda binti wa mlinzi wake wa gereza ambaye alimtembelea alipokuwa amefungwa," waliripoti.

Kabla ya kifo chake, inadaiwa kuwa alimwandikia barua iliyosainiwa 'From your Valentine,' usemi ambao bado unatumika hadi leo.

"Ingawa ukweli wa hadithi za Valentine haueleweki, hadithi zote zinasisitiza rufaa yake kama mtu mwenye huruma, shujaa na muhimu zaidi wa kimapenzi," History Classics ilisema.

Hadithi nyingine ya kawaida inasema kwamba Mtakatifu Valentine alikaidi maagizo ya mfalme na wanandoa wa ndoa kwa siri kuwaepusha waume zao kutoka kwa vita.

Ni kwa sababu hii kwamba siku yake ya sikukuu inahusishwa na upendo.