Eric Omondi adai rais Ruto ndiye kiongozi wa Gen Z, afichua mipango ya kisiasa ya vijana

"Kila wakati akiongea, akifanya chochote, inawasha hasira. Yeye ndiye anafanya Gen Z wanachemka," Eric alisema.

Muhtasari

•Eric Omondi alikanusha kuwa kiongozi wa Gen Z na kudai kuwa rais mwenyewe ndiye anayechochea harakati hiyo.

•Alisema kuwa upinzani kushirikisha katika serikali ni baraka kwani imesaidia kutenganisha tabaka la kisiasa na raia wa kawaida.

Eric Omondi
Eric Omondi
Image: HISANI

Mchekeshaji na mwanaharakati maarufu wa Kenya Eric Omondi alizuru studio za Radio Jambo Alhamisi asubuhi ambapo alishiriki mazungumzo mafupi na watangazaji Gidi na Ghost.

Miongoni mwa mambo aliyozungumza mtangazaji huyo wa zamani wa redio ni pamoja na hali ya kisiasa nchini kwa sasa, maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z, mawaziri wapya walioteuliwa na mipango ya kisiasa ya vijana wa Kenya.

Eric aliulizwa ikiwa kwa njia yoyote anahusika katika uongozi wa vuguvugu la Gen Z ambalo limehusika pakubwa katika maandamano ya hivi majuzi. Hata hivyo, alikanusha kuwa kiongozi wa Gen Z na kudai kuwa rais mwenyewe ndiye anayechochea harakati hiyo.

"Apana. Kiongozi wa Gen Z ni William Ruto. Kila wakati akiongea, akifanya kitu, kila kitu inawasha hasira. Yeye ndiye anafanya Gen Z wanachemka. Kama unatafuta kiongozi wa Gen Z, na William Samoei Ruto,” Eric alisema.

Huku akizungumzia wateule wa baraza la mawaziri, na upinzani kushirikishwa katika serikali ya Kenya Kwanza, mchekeshaji huyo alisema kuwa ni baraka kwani imesaidia kutenganisha tabaka la kisiasa na raia wa kawaida.

“Tuna furaha sana kwa sababu wamekuja upande mmoja, tabaka la kisiasa na wanasiasa wakongwe. Sasa tumebaki na wakenya. Wakenya sasa wako upande mmoja. Sasa sisi ndio upinzani,” alisema.

Aliongeza,” Sisi tuko wengi lakini hatujajipanga, sasa tutajipanga. Tukianza kujipanga, mtupatie nafasi. Tunaenda kuchukua ID na kujiandikisha kupiga kura.”

Katika miaka ya hivi majuzi, mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show amejihusisha sana na siasa za ndani na amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali.