Peter Mutuku ,41, kutoka Kitengela alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na ndugu yake mkubwa Bernard Mutinda ,46, ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.
Peter alisema uhusiano wake na nduguye uliharibika Januari mwaka huu wakati alipozozana naye kuhusu shamba.
"Mwaka jana mwezi wa kumi tulienda nyumbani tukaongea na wazazi, kuna shamba walikuwa wanauza.Tulikubaliana wakati itakuwa inauzwa kila mtu awe pale. Babangu na ndugu yangu alituchezea chini ya maji, wakauza na kugawana pesa," Peter alisema.
Aliongeza, "Nilienda kwake akanieleza waliuza shamba bila kutuarifu. Nikaamuuliza kwa nini waliuza ilhali tulikuwa tumekubaliana kila mtu angekuwa wakati wa kuuzwa. Nilimkashifu na kumtusi, nilienda kulalamika kivyangu."
Bw Bernard alipopigiwa simu alipinga madai ya kushirikiana na baba yao kuuza shamba ya familia.
Aidha, alimshtumu nduguye mdogo kwa kuwa mlevi na kuzozana na wengine wakati akinywa pombe.
"Mimi ni mtu mzima. Mimi ndiye mkubwa wake. Shida ilipotokea, huyo jamaa ni mtu wakati akinywa pombe ndio anataka kutafuta suluhu. Mwaka uliopita ulipoisha, alikosana na bibi yake, lakini watoto wake walikuja kwangu. Baadaye alikuja kwangu akiwa mlevi. Nikamwambia aache ulevi na awache kuzozana na watu akiwa mlevi," Bernard alisema.
Aliendelea, "Mambo ya shamba namshangaa sana. Wakati shamba iliuzwa, yeye mwenyewe ndiye alikuja kunijulisha shamba imeuzwa."
Peter alisema, "Ndiyo nilimwambia shamba inauzwa polepole. Tukapanga tuwe na mkutano nyumbani, tukasema iliyobaki bila watu wengine kujua. Yeye mwenye aliniambia alitumiwa pesa."
Alikiri kumtumia mkubwa wake cheche za maneno na akaeleza kwamba alifanya hayo kutokana na hasira.
"Ukinywa pombe, weka kwa tumbo moja. Mimi sina shida na wewe, lakini ukinywa pombe, weka kwa tumbo moja. Usiwahi kuniongelesha ukiwa mlevi. Wewe ata huwa unashughulika aje na familia. Tabia zako mbovu, nani atazungumza na wewe," Bernard alimjibu kwa hasira kabla ya kukata simu.
Peter alimalizia kwa kusema, "Mimi nilitaka nikuombe msamaha hayo yaishie hapo. Wakati tunafanya maamuzi mengine kwa familia ni muhimu kufahamisha kila mtu, iwe mlevi ama nani lazima ahusishwe."
Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?