"Alikuwa na matatizo ya akili" Akothee afichua sababu halisi ya kuvunja ndoa na Omosh

"Alikuwa na changamoto za afya, matatizo ya akili hivi, sitasema ni mwendawazimu lakini alikuwa na shida ya kiakili," Akothee alisema.

Muhtasari

•Akothee alisema alikuja kugundua mengi ambayo mzungu huyo alimficha awali, na akabainisha hangeweza kuvumilia uwongo huo.

•Mama huyo wa watoto watano hata hivyo alibainisha kuwa kama mambo mengine mengi, hata ndoa pia huisha.

Akothee na aliyekuwa mumewe wake Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akoth amesema kuwa mume wake wa zamani Denis Schweizer almaarufu Mister Omosh alimficha mambo mengi sana kabla ya wao kufunga ndoa Aprili mwaka jana, jambo ambalo lilimkasirisha.

Akizungumza kwenye mahojiano na mtangazaji Gidi Ogidi kwenye kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alifichua kwamba alikuja kugundua baadaye mambo ya ndani ambayo mzungu huyo kutoka Uswizi alimficha awali, na akabainisha hangeweza kuvumilia uwongo huo.

Akothee alisema mume wake wa zamani alikuwa akipambana na matatizo fulani ya kiakili lakini hakuwa amemweleza kuhusu hilo kabla ya wao kufunga ndoa rasmi.

“Siwezi sema alikuwa mtu wa mzaha, lakini yale ambayo nilikuja kugundua baadaye ni mambo singeweza kuketi nayo kwa sababu alinificha. Kule kunificha ndio kuliniumiza nikasema kama umenificha kwa wakati huu, ni mangapi utanificha baadaye, nitakuwa naishi vipi? Nitakuwa nakuamini vipi?,” Akothee alisema.

Aliendelea, “Kilichofanya niachane naye ni kwamba hakuniambia ukweli wake wa ndani kwamba alikuwa na changamoto za afya, ile ya kwamba ana yale magonjwa ya akili hivi, sitasema ni mwendawazimu lakini alikuwa na shida ya kiakili. Alikuwa na bipolar hivi. Aliponiambia nikamuuliza kwa nini hakuniambia kama hatujafunga harusi nikajiaibisha mbele ya watu.

Mama huyo wa watoto watano hata hivyo alibainisha kuwa kama mambo mengine mengi, hata ndoa pia huisha.

Hata hivyo alilalamika kuhusu wanaume wanaofanya mzaha na masuala ya mahusiano, na kuwataka kuwa waangalifu hasa wanaposhughulika na wanawake wa miaka 40 iliyopita.

“Hata Big-G ikiisha utamu, lazima uteme. Wajua ndoa ni mahusiano ya watu wawili.Unakutana na mtu ambaye ulikutana naye na meno 32, hujui atokako na aendako, hujui anaendelea vipi. Wewe wataka mapenzi, huyu mtu hujui anataka nini.

Wajua hii miaka yangu ya 40 hivi hatujui mzaha, hatupendi mzaha. Kwa hiyo kama unachumbia mwanamke katika miaka yake ya 40, ni wakati wa jeraha, usifanye mzaha nasi kuhusu ndoa. Ata kama unataka kusema nataka maji, tunajua unataka kutuoa. Tunakuamini,” alisema.

Akothee aliachana na Omosh wakati fulani mwezi wa Juni, takriban miezi miwili baada ya kufanya harusi ya kupendeza na mzungu huyo jijini Nairobi, Kenya.