Asante sana! Gidi na Ghost Asubuhi ndiyo shoo ya asubuhi maarufu zaidi Kenya

Watangazaji uwapendao, Gidi na Ghost wameapa luwa wako tayari kukupa bora zaidi.

Muhtasari

•Utafiti wa hivi majuzi uliofanywa na IPSOS ulithibitisha kuwa shoo hiyo ndiyo maarufu zaidi ya asubuhi humu nchini. 

•Radio Jambo inakuahidi mengi zaidi makubwa na mazuri  katika Gidi na Ghost Asubuhi na vipindi vyetu vingine

Image: RADIO JAMBO

Ni wazi kwamba kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo ndicho kipindi kikubwa zaidi cha redio cha asubuhi nchini Kenya.

Utafiti wa hivi majuzi uliofanywa na shirika la IPSOS ulithibitisha kuwa shoo hiyo ambayo hupeperushwa kila siku za wiki kutoka saa kumi na mbili asubuhi hadi saa nne asubuhi ndiyo shoo maarufu zaidi ya asubuhi humu nchini. 

Kutokana na hilo, Radio Jambo ingependa kutoa shukrani za dhati kwa wasikilizaji wetu wote nchini kote kwa sapoti  yenu isiyoisha. Ushindi huu si wa Radio Jambo pekee, bali pia mamilioni ya mashabiki wetu waaminifu ambao wametufanya tuwe nambari moja.

Kipindi hiki kinapeperushwa na mabingwa wawili wa utangazaji, Joseph Ogidi almaarufu Gidi na Jacob Ghost Mulee ambao wamekuwa na muungano nzuri kwa miaka mingi ambayo wamefanya kazi pamoja.

Mtangazaji Ghost' Mulee aliambia mwandishi Samuel Maina kuwa kufanya kazi kama mtangazaji mwenza wa Gidi imekuwa ni safari nzuri ya kufarahisha.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Harambee Stars alibainisha kuwa ni mara chache tu  ametofautiana na Gidi kwa takriban miaka kumi na mitano iliyopita ambayo wamekuwa wakifanya kazi pamoja.

"Tumefanya kazi vizuri kwa miaka kumi na nne bila wasiwasi wowote.  Hakuna kukorofishana, huwa ni masuala ya kazi, kama kuna tofauti huwa za kikazi na baada ya pale tunatoka tunaenda zetu," alisema.

Ghost alilinganisha uhusiano wake wa kikazi na Gidi na ndoa imara.

Hata hivyo, alikiri kuwa kama ndoa nyingine yoyote, hakujakosa changamoto katika 'ndoa' yake na mtangazaji huyo. Alibainisha kuwa mara zote Gidi huwa tayari kumrekebisha kila anapokosea kazini.

"Ni ndoa ambayo huwezi kuiacha isipokuwa uamue hivyo. Tumekaa kwa hii ndoa miaka kumi na minne. Imekuwa ni changamoto. Gidi ana haiba tofauti na yangu. Lakini nampenda kwa sababu tukifanya naye kazi, unapata saa zingine mimi ni mtu wa mzaha, nikitoka laini ananirejesha kama mwalimu mkuu," alisema.

Ghost pia alizungumzia kitengo maarufu kwenye kipindi chao 'Patanisho' na kusema kuwa inawapa furaha nyingi kusaidia watu kurudiana.

"Ni raha yetu waliokosana wakiweza kupatana na kurudiana. Hakuna haja ya kukaa na kinyongo moyoni. Kama umekosea mtu muombe msamaha. Kama amekukosea nawe kubali msamaha," alisema.

Radio Jambo inakuahidi mengi zaidi makubwa na mazuri  katika Gidi na Ghost Asubuhi na vipindi vyetu vingine. Watangazaji uwapendao, Gidi na Ghost wameapa luwa wako tayari kukupa bora zaidi.

Kwa mara nyingine, shukran sana na uendelee na sapoti..