Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo amesisitiza kwamba hakuwa nyumbani wakati rafiki yake Jeff Mwathi alikumbana na kifo chake takriban miezi mitatu iliyopita.
Katika mahojiano maalum na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Radio Jambo, DJ Fatxo alidai kwamba alikuwa amezimia ndani ya gari lake baada ya kubugia vinywaji kadhaa na wenzake usiku uliopita.
Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alisema kuwa mlinzi wa lango lao ndiye aliyemjulisha kuhusu mtu ambaye alikuwa amejitupa chini wakati alipofika nyumbani mwendo wa saa tatu asubuhi ya usiku Jeff alifariki.
"Kawaida nilikuwa napark first floor, nikasema nisipark hapo nione ni nani huyo amejiangusha kutoka ghorofa ya 12," alisimulia.
Alisema baada ya kuegesha gari lake, hakuelekea kwa nyumba yake mara moja bali aliutazama mwili wa marehemu kwa mbali.
"Baada ya kuegesha, mwili ulikuwa karibu. Kuna nguzo ya jengo ilikuwa inazuia. Niliona kichwa mahali lakini kando kulikuwa na nyama nyama zimetapakaa. Nguzo zilinizuia hata kuona mwili, niliona tu nywele kidogo mahali kichwa ilikuwa," alisema.
Alisema kuwa aliogopa sana kutazama mwili huo kwa vile hakuwa amezoea kutazama miili ya watu waliokufa.
"Mimi naogopa sana. Mwili wenye nishaona kwa mochari ni wa nyanya yangu tu," alisema
Alisema kutokana na uoga huo hakuutazama mwili huo moja kwa moja badala yake aliutazama kwa haraka.
"Kitu pekee ambacho niliona ni kichwa kilichoharibiwa pande moja na nikaona mtu hana suruali. Nilishika kichwa changu kama naenda kwa sababu singeangalia sana. Sijawahi weza kuangalia. Naogopa," alisema.
Alisema wakati huo polisi walikuwa wakisubiri kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Baada ya hapo kutazama mwili alisema alielekea kwa nyumba yake huku akiwaza kwanini mtu achukue hatua hiyo.