Gidi aonyesha nyakati za mwisho za hisia za mpwa wake mdogo aliyeaga, Pendo (+video)

Gidi alimpoteza mpwa wake, Princess Pendo siku ya Jumapili jioni.

Muhtasari

•Gidi Ogidi ameshiriki baadhi ya dakika za mwisho za mpwa wake aliyefariki kutoka siku moja kabla ya kifo chake.

•Katika video ambayo Gidi alichapisha, marehemu Pendo anasikika akikariri mstari wa Biblia kutoka Zaburi 23:6. 

Mtangazaji Gidi Ogidi

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, Gidi Ogidi ameshiriki baadhi ya kumbukumbu za mwisho za mpwa wake aliyefariki kutoka siku moja kabla ya kifo chake.

Gidi alimpoteza mpwa wake, Princess Pendo siku ya Jumapili jioni.

Pendo ambaye ni binti pekee wa dadake Gidi, Lydia Oyoo alikata roho mwendo wa saa mbili usiku, siku ya Jumapili katika Hospitali ya Metropolitan. Alikuwa na umri wa miaka saba tu.

Gidi sasa amefichua kwamba siku moja kabla ya kukutana na kifo chake, marehemu Princess Pendo alikuwa amehudhuria ibada ya kanisa na hata alikariri mstari wa Biblia mbele ya waumini.

"Huyu ni mpwa wetu Princess Pendo akikariri mstari wa Biblia Jumamosi iliyopita katika kanisa. Aliaga dunia siku iliyofuata (Sunday iliyopita)😥😥😥," aliandika chini ya video ya msichana huyo mdogo akikariri mstari wa Biblia.

Katika video ambayo mtangazaji huyo mahiri alichapisha, marehemu Pendo anasikika akikariri mstari wa Biblia kutoka Zaburi 23:6. 

"Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu, nami nitakaa nyumbani mwa BWANA milele," alikariri kwa Kiingereza.

Gidi alitangaza habari za kifo cha mpwa huyo wake siku ya Jumatatu asubuhi kupitia ukurasa wake wa Instagram.

"Tulikuwa na usiku mrefu lakini wacha nishukuru hospitali, jirani yangu Wakili na marafiki ambao walituunga mkono katika mchakato wa kuhamisha mwili wake hadi chumba cha kuhifadhi maiti," aliandika.

Siku ya Jumanne, alitoa shukran za dhati kwa kanisa la Nairobi East SDA kwa kusaidia katika kumfariji dada yake aliyefiwa na bintiye huku akifichua jinsi ya kusaidia familia katika mipango ya mazishi.

"Tumefungua bili ya malipo hapa chini kwa marafiki na tutapenda kusaidia Lydia kumpa binti yake, Princess Pendo mazishi yafaayo. Asanteni wote kwa jumbe zenu za rambirambi," alisema chini ya bango alilochapisha.

"Kumsaidia mama yake 🙏🏿 Nambari ya malipo: 891300 Nambari ya Akaunti: 63501 Piga *483*50*63501#," alisema.

 Sote katika Radio Jambo tunaitakia familia ya Gidi amani na nguvu na wanapomuomboleza mmoja wao. Roho ya Pendo ipumzike kwa amani.