"Hakuonyesha mawazo ya kujiua" Ghost Mulee azungumzia mkutano wake na marehemu Jeff Mwathi

"Jeff alijawa na maisha na mwenye maono makubwa, nilitangamana naye," Ghost alisema.

Muhtasari

•Ghost alifichua kwamba alikuwa na bahati kukutana na kutangamana naye kabla ya kukumbana na kifo chake kibaya.

•Aidha ,kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alitilia shaka madai kwamba Jeff alikuwa na mawazo ya kujitoa uhai.

Mtangazaji Ghost Mulee na marehemu Jeff
Image: JACOB GHOST MULEE

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob Ghost Mulee ameendelea kumuomboleza kijana Geoffrey Mwathi almaarufu Jeff ambaye alifariki katika mazingira tatanishi mwezi uliopita.

Jeff alifariki mnamo Februari 22 na ripoti iliyoandikishwa katika kituo cha polisi iliashiria kuwa alijitoa uhai kwa kuruka  kupitia dirisha la nyumba ya mwimbaji maarufu wa Mugithi, Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo.

Huku akiungana na Wakenya kudai haki kwa mpwa huyo wa staa wa Mugithi Samidoh, Ghost alifichua kwamba alikuwa na bahati kukutana na kutangamana naye kabla ya kukumbana na kifo chake kibaya.

"Jeff alijawa na maisha na mwenye maono makubwa, nilitangamana naye," Ghost alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aidha ,kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alitilia shaka madai kwamba Jeff alikuwa na mawazo ya kujitoa uhai.

"Hakuwahi kwa wakati mmoja kuonyesha mawazo yoyote ya kujiua," alisema.

Walioandikisha taarifa katika kituo cha polisi walieleza kuwa kijana huyo wa miaka 23 aliwahi kuwa na mawazo ya kujitoa uhai miaka ya nyuma. Walidai kuwa aliruka kutoka orofa ya kumi ya jengo hilo na kukatisha maisha yake papo hapo bila ufahamu wa watu ambao alikuwa nao ndani ya nyumba ya DJ Fatxo.

Hali kuhusu kifo cha Jeff na jinsi kilivyoshughulikiwa hata hivyo imetiliwa shaka sana na Wakenya wenye hasira haswa kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakiwaagiza wapelelezi kufanya uchunguzi wa kina.

Siku ya Ijumaa, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliahidi uchunguzi wa kina katika kesi ya kifo cha kijana huyo wa miaka 23.

Taarifa iliyotolewa na DCI siku ya Ijumaa ilisema kitengo cha kuchunguza mauaji cha idara hiyo kilichukua kesi ya kifo cha kijana huyo ambaye ni binamu ya Samidoh kufuatia agizo la mkuu wa DCI, Bw Mohamed Amin.

"Umma umehakikishiwa kuwa hakuna jiwe ambalo halitapinduliwa katika upelelezi wa kesi hii na mtu yeyote atakayebainika kuhusika na kifo hicho atakabiliwa na mkono wa sheria," taarifa ya DCI ilisoma.

Kufuatia hilo, wapelelezi walitoa wito kwa umma kutoa taarifa yoyote ambayo itasaidia katika uchunguzi.