'Ilifika wakati singeweza kunyonyesha,' Carrol Sonnie afunguka jinsi alivyopambana na msongo wa mawazo

Muhtasari

•Muthoni alikiri kuwa matukio yaliyofuata baada ya kutangaza kutengana kwake na Mulamwah yalimuathiri vibaya kiasi cha kwamba alishindwa kunyonyesha bintiye.

•Amesema kuwa wazazi wake pamoja na baadhi ya marafiki na mashabiki walimsaidia sana kupambana na msongo wa mawazo ambao ulikuwa umemuathiri.

Carrol Sonnie katika studio za Radio Jambo
Carrol Sonnie katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mwigizaji Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonnie alilemewa na hisia studioni zetu alipokuwa anasimulia kuhusu athari za baada ya kutengana na aliyekuwa mpenzi wake mchekeshaji Mulamwah.

Akizungumza na Massawe Jappani katika kitengo cha 'Ilikuaje?', Muthoni alikiri kuwa matukio yaliyofuata baada ya kutangaza kutengana kwake na Mulamwah yalimuathiri vibaya kiasi cha kwamba alishindwa kunyonyesha bintiye.

"Kusema kweli, sasa nimepona. Iliniathiri sana. Ilifika wakati hata singeweza kunyonyesha mtoto. Maziwa ilikuwa imeisha. Mamangu alikuwa anachukua simu yangu ili nisisome jumbe. Niliathiriwa na msongo wa mawazo. Ni mwanamke tu ataweza kuelewa hali hiyo. Nashukuru kuwa mtoto wangu anaendelea vizuri lakini hapo awali ilikuwa ngumu kwake," Muthoni alisema.

Muthoni alisema wazazi wake pamoja na baadhi ya marafiki na mashabiki walimsaidia sana kupambana na msongo wa mawazo ambao ulikuwa umemuathiri.

Mwigizaji huyo ameweka wazi kuwa tayari ameweza kusonga mbele na maisha yake. Hata hivyo amekiri kuwa anampeza sana Mulamwah katika maisha ya binti yao.

"Kusema kweli nilitaka mahusiano  yetu yafanye kazi. Lakini kwa kuwa mambo yalienda jinsi yalivyoenda lazima tusonge mbele na maisha na tuzoee. Napeza uwepo wake hasa kwa maisha ya mtoto wangu. Ningependa ahusike zaidi katika malezi," Muthoni alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja amefichua kuwa kwa sasa hawazungumzi na baby daddy wake. Pia alifichua kuwa mara ya mwisho ya Mulamwah kuona bintiye na akiwa na umri wa miezi miwili.