Carol Muthoni ataja mambo aliyojifunza kutokana na kuvunjika kwa mahusiano yake na Mulamwah

Muhtasari

•Mama huyo wa mtoto mmoja alisema walifanya makubaliano ya pamoja na Mulamwah kuvunja mahusiano yao baada ya kugundua yalikosa uhai.

•Alisema amejifunza kujipenda zaidi kuliko mpenzi wake huku akimshtumu Mulamwah kwa kukosa kumpa mapenzi sawa na yale aliyompatia mwenyewe. 

Carol Muthoni katika studio za Radio Jambo
Carol Muthoni katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mwigizaji Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonnie alitembelea studio zetu siku ya Jumatatu ambapo alifunguka mengi kuhusu mahusiano yake na mchekeshaji Mulamwah.

Akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japanni, Muthoni alifichua kuwa kiini kikuu cha kuvunjika kwa mahusiano yao ni ukosefu wa uaminifu.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema walifanya makubaliano ya pamoja na Mulamwah kuvunja mahusiano yao baada ya kugundua yalikosa uhai.

"Kusema kweli sote wawili tulikaa chini tukaongea na tukagundua kuwa  mahusiano yetu hayakuwa na mwelekeo.Tulikubaliana kutengana kwa njia nzuri. Tulikuwa natofauti zetu na hatungeweza kuendelea. Tulikuwa tunarudi nyuma. Uaminifu ulikosekana," Muthoni alisema.

Muthoni alikiri kuwa alipata mafunzo mengi katika kipindi cha miaka minne ambacho alikuwa kwenye mahusiano na Mulamwah.

Alisema amejifunza kujipenda zaidi kuliko mpenzi wake huku akimshtumu Mulamwah kwa kukosa kumpa mapenzi sawa na yale aliyompatia mwenyewe. 

"Kosa ambalo siwezi taka kurudia ni kupenda mtu mwingine kuliko ninavyojipenda. Nimejifunza nijipende zaidi ndio nipende mtu mwingine," Muthoni alisema.

Mwigizaji huyo pia alisema amejifunza kujisimamia mwenyewe na kutotegemea mtu mwingine kamwe maishani.

Muthoni aliweka wazi kuwa hakuwahi tegemea baba ya mtoto wake wakati walipokuwa  kwenye mahusiano.

"Nimejifunza kuwa nataka nifanye kazi nipate pesa zangu. Mimi sijawahi kumtegemea mtu yeyote. Sijawahi tegemea mwanaume yeyote. Ata Mulamwah ukimpigia simu umuulize kama nimewahi kumuomba ata pesa ya nywele, huwa sifanyi hilo," Alisema.

Muthoni alikiri kuwa alimpenda mchekeshaji huyo sana kuliko jinsi alivyojipenda yeye. Hata hivyo aliweka wazi kuwa hana majuto yoyote kwa kumpenda.