Mwanavlogu Kelvin Kinuthia azungumza kuhusu suala la jinsia yake

Muhtasari
  • Kinuthia alisema kuwa jeni za familia yake na lishe bora zimechangia sana katika unene wa makalio na kiuno chake
Kelvin Kinuthia katika studio za Radio Jambo
Kelvin Kinuthia katika studio za Radio Jambo
Image: MERCY MUMO

Mwanavlogu Kelvin Kinuthia amepatia watu uhuru wa kumtambulisha kama mwanaume ama mwanamke.

Akizungumza na Massawe Japanni katika kipindi cha Bustani la Massawe, Kinuthia alisema hana tatizo lolote kutambulishwa na jinsia yoyote ile.

"Ningependa kuitwa Kinuthia tu, hiyo ni sawa. Mi husema kile mtu atataka kuniita,ni sawa. Mimi niko sawa. Ukiniita mwanamke siweze kuhukumu kwa sababu hata navalia kama mwanamke," Alisema.

Mwavlogu huyo hata hivyo alikataa kuweka wazi jinsia yake halisi ambayo imeendelea kuibua utata mwingi miongoni mwa watumizi wa mitandao ya kijamii.

Kinuthia alisema kuwa jeni za familia yake na lishe bora zimechangia sana katika unene wa makalio na kiuno chake.

"Sijawahi enda kuangaliwa mbona nimeumbwa hivi. Lakini nadhani ni kitu iko kwa familia. Ata mama ako hivi tu. Pia ni kulula vizuri, kuleni vizuri," Alisema.

Alisema kuwa atazungumzia suala la jinsia yake halisi kikamilifu wakati atajihisi kuwa tayari.