"Niko hapa kukufanya ujivunie mama," Mwanavlogu Kelvin Kinuthia amsifia mama yake

Muhtasari

Kelvin Kinuthia
Image: Mercy Mumo

Mwanavlogu mashuhuri Kelvin Kinuthia amekiri wazi kuwa hofu yake kubwa maishani ni kumpoteza mama yake mzazi.

Akizungumza katika kipindi cha Bustani la Massawe, kitengo cha Ilikuaje?, Kinuthia alisema kuwa anamthamini sana mamake kwa kuwa amekuwa naye katika hatua zote za maisha.

Mwanavlogu huyo mwenye umri wa miaka 21 alifichua kuwa alimpoteza baba yake wakati alipokuwa katika darasa la tatu na mamake akachukua majukumu yote tangu wakati huo.

"Nilimpoteza babangu nikiwa katika darasa la tatu. Sikuathirika sana kwa kuwa mama yangu ni kama baba tu," Kinuthia alisema.

Kinuthia alisema kuwa mamake ni shabiki mkubwa wa  sanaa yake licha ya ukosoaji mkubwa ambao amekabiliana nao kwenye mitandao ya kijamii tangu alipopata umaarufu.

Alieleza kuwa tabia ya kuvalia mavazi ya kike na kujirembesha haikuanza hivi majuzi kwani kitambo alipendelea kuchukua mavazi ya mamake na kuyavaa.

"Nilikuwa naona watu wakikaa vizuri na makeup. Niliona picha na video zao zikikaa vizuri nikasema lazima nijaribu hilo siku moja. Nilianza kitambo. Nilikuwa nachukua nguo za mama na wigs najibamba nazo. Kitambo hakuipenda tabia hiyo lakini kadri siku zilivyosonga alikubali na akawa sawa nayo," Alisema.

Mwanablogu huyo anamshukuru sana mama yake kwa kumuunga mkono katika hatua zote za maisha yake huku akimhakikishia upendo mkubwa alionao kwake.

"Ningependa mama ajue kuwa nampenda sana na namshukuru kwa kuniunga mkono. Niko hapa kukufanya ujivunie mama," Alisema.