DJ Fatxo afunguka kwa nini alimwaga machozi studioni wakati akisikiliza sauti ya Mama Jeff

"Ni kwa sababu nimehisi vibaya sana. Ukiskia vile mama ameongea nashangaa kama utu utawahi kurudi," alisema.

Muhtasari

•Massawe alicheza mahojiano ya simu na mamake Jeff Mwathi ambapo alisema maneno makali dhidi ya mwanamuziki huyo na hata kumlaani yeye na familia yake.

•DJ Fatxo alilalamika kwamba familia ya marehemu tayari imehitimisha kwamba alihusika katika mauaji yake ilhali kulingana naye, sio kweli.

awezwa na hisia ndani ya studio za Radio Jambo.
DJ Fatxo awezwa na hisia ndani ya studio za Radio Jambo.
Image: RADIO JAMBO

Staa wa Mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo alikuwa mgeni wetu Jumatatu wakati wa kipindi cha Bustani la Massawe.

Wakati wa mahojiano, mtangazaji Massawe Japanni alicheza mahojiano ya simu yaliyorekodiwa na mamake Jeff Mwathi ambapo alisema maneno makali dhidi ya mwanamuziki huyo na hata kumlaani yeye na familia yake.

Wakati sauti ya mamake Jeff ikiendelea kucheza, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 27 alionekana kuguswa na hata kuangua kilio. Baadaye Massawe alimuuliza kwa nini alilia huku  na akasema;-

"Ni kwa sababu nimehisi vibaya sana. Ukiskia vile mama ameongea nashangaa kama utu utawahi kurudi," alisema.

Alishangaa kwanini mamake Jeff hakutambua kuwa alitaka kumsaidia mwanawe kabla ya tukio hilo na kusisitiza kwamba hakumuua. Alidai ikiwa kweli alikuwa na nia ya kumuua, ni mantiki asingempeleka nyumbani kwake.

DJ Fatxo alilalamika kwamba familia ya marehemu tayari imehitimisha kwamba alihusika katika mauaji yake ilhali kulingana naye, sio kweli.

Katika mahojiano ya simu na Massawe, mamake Jeff alisisitiza kwamba anaamini mwimbaji huyo wa Mugithi alihusika.

"Hata yeye anafaa kupitia kitu kama hiyo. Alifanya vibaya sana, kuua mtoto wa mtu hivo hadharani," Mamake Jeff alisema.

Mama yake Jeff ambaye alisikika kuwa na kinyongo sana na mwanamuziki huyo ambaye hivi majuzi aliondolewa mashtaka ya mauaji ya kijana huyo wa miaka 23 aliendelea kumlaani pamoja na familia yake.

Fatxo hata hivyo alisisitiza kwamba marehemu alikuwa rafiki yake na kubainisha hakuwa na sababu yoyote ya kumdhuru.

"Jeff alikuwa rafiki yangu. Sioni sababu yangu kumuua," alisema.

DJ Fatxo alifichua kuwa alikuja kujuana na kijana huyo wa miaka 23 mwaka wa 2021 kupitia rafikiye mwanamke ambaye alikuwa akimuuzia viatu. Wakati huo alikuwa akivuma kutokana na nyimbo maarufu alizokuwa ameachia.

"Jeff alikuwa na duka la viatu. Napenda mambo na fashion, nilienda pale nikapata mwanadada kwa jina Faith Mutanu. Sikujua duka ni kwa Jeff. Nilikuwa nimenunua viatu vya zaidi ya laki moja," Fatxo alisimulia.

Aliongeza, "Jeff alisema shukran ati nimekuwa nikimpromote sana. Sikuacha kuwa customer wake. Tulipopatana alipiga picha na mimi. Hapo akaniambia Samidoh ni mjomba wake. Mimi nikatupilia mbali kwa kuwa sikuona mengine ya kuzungumza naye."

Alisema Jeff alimpata pale dukani mara kadhaa baada ya mkutano wa kwanza ila hawakuwahi jenga urafiki wa karibu.